Kube
Juu ni Kubenea akinyanyuliwa mkono na Lowassa kunadiwa kwa kiti cha Ubunge Ubungo mwaka 2015. Chini ni makala aliyowahi kuandika Kubenea kuhusu Edward Lowassa.
Mabilioni yatengwa kumsafisha Lowassa


Na Saed Kubenea

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya mkataba tata wa Richmond, Edward Lowassa ameelezwa kuwa na mradi wa karibu Sh. 8 bilioni wa “kujisafisha” na kumwingiza ikulu.

Lowassa alipoulizwa na gazeti hili kuhusu mradi huo, alijibu kwa mkato, “Mimi sijui.”
MwanaHALISI limeelezwa kwamba fedha za “kumsafisha” Lowassa zimeahidiwa na swahiba wake, Rostam Aziz ambaye wamesimama pamoja muda wote wa sakata la kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond iliyothibitika kuwa feki.

Richmond ilipewa mkataba wa kufua umeme ikiwa haina fedha, wataalam wala uzoefu katika eneo hilo; huku nyaraka zilizopo juu ya kashfa hiyo zikionyesha kuwa mkataba ulipatikana kwa njia ya upendeleo – tuhuma ambazo zinamwangukia Lowassa.

Taarifa zinasema mabilioni hayo ya shilingi yamelenga kutumika kulegeza wajumbe wa vikao vya maamuzi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hasa kuelekea, na wakati wa mkutano mkuu ndani ya chama hicho ambao utafanyika mwaka kesho.

Fedha hizo pia zinadaiwa kulenga kuyumbisha jumuiya za CCM – Umoja wa Wanawake (UWT), Jumuiya ya wazazi na Umoja wa Vijana (UV-CCM).

Wengine ambao wanadaiwa kulengwa katika hatua ya kushawishi, kulegeza na kushirikisha katika mradi wa kusafisha Lowassa ni wabunge, vyombo vya habari na waandishi wa habari mmojammoja.

“Mradi wa kumsafisha Lowassa” umeelezwa kuwa chini ya kundi la watu watano. Mbali na Lowassa mwenyewe na Rostam, wengine waliotajwa ni Andrew Chenge, Makongoro Mahanga na Peter Serukamba.

Chenge ni mbunge wa Bariadi Magharibi; Mahanga ni mbunge wa Segerea na Serukamba ni wa Kigoma Mjini. Taarifa zinasema tayari baadhi ya wajumbe wa kundi hilo wamefanikiwa kushika nafasi za juu za Kamati za Kudumu za Bunge.
Walioshika nafasi hizo ni Lowassa (Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama) na Serukamba (Miundombinu).

Gazeti hili limeelezwa kuwa mgogoro unaoendelea ndani ya UV-CCM, unatokana na “kasi ya mbio za Lowassa kugombea nafasi muhimu” ndani ya chama chake na baadaye urais.

Kwa wiki mbili sasa, viongozi wa vijana wamekuwa wakisutana, kulaumiana na kutuhumiana kujenga makambi ndani ya umoja huo. Wiki iliyopita walimrukia waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye wakimtuhumu kuhujumu chama “kwa kuzungumza nje ya vikao.”

“Sikiliza bwana ee, vurumai hii ya vijana ni ya kutafuta kujenga kundi la kumsafisha Lowassa. Wapo wanaofanya kazi hiyo kwa kujua na wapo wanaofanya hivyo bila kujua,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM.

Hatua ya baadhi ya viongozi wa vijana, kurukia kila wanayeona ana uwezekano wa kupinga Lowassa na kundi lake, inaelezwa kutokana na waliokuwa wapinzani wao wakuu kubaki serikalini na wao (akina Lowassa) kuwa nje ya utawala.
Wanaotajwa kuwa serikalini, lakini wanadaiwa kuwa wapinzani wa Lowassa katika mgawanyiko wa wanaopinga ufisadi na wanaoutetea, ni pamoja na Samwel Sitta, ambaye hivi sasa ni waziri wa Afrika Mashariki.
Wengine ambao akina Lowassa hawakutegemea kuwemo serikalini, ni waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, Benard Membe; naibu waziri wa ujenzi, Dk. Harisson Mwakyembe na mkuu wa wilaya ya Masasi, Nape Nnauye.
Lowassa hakuwa na simile pale alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusu “mradi wa kujisafisha.”

Swali: Mheshimiwa, tumepata taarifa kuwa una mradi wa Sh. 8 bilioni kwa ajili ya “kujisafisha kisiasa.” Je, hii ni kweli?
Lowassa: Muulizeni huyo mpuuzi aliyewaambieni.

Swali: Gazeti linakuliza wewe kwa kuwa ndiyo mwenye mradi.
Lowassa: Mimi sijui. Sitaki kusikia mambo ya kijinga…”

MwanaHALISI liliripoti katika toleo lake la Machi 9 – 15 mwaka huu, chini ya kichwa cha habari kisemacho, “ Siri ya Edward Lowassa nje,” juhudi za mbunge Beatrice Shelukindo “kumsafisha” Lowassa.

Katika ujumbe wake wa maandishi kwa mbunge mwenzake, Pindi Chana, Shelukindo alisema ameambiwa na Nabii Joshua wa Nigeria kuwa “rais ajaye ni Edward Lowassa” na kwamba maisha yake ya nyuma yanayomhusisha na kashfa ya ufisadi, “si kitu.”

Joto la Shelukindo katika mawasiliano haya lilitokana na kile alichoeleza kuwa, “Mungu ni wa ajabu. Lowassa ameniombea kura pasipo maelezo. Ameandaa lunch na dinner (vyakula vya mchana na usiku) ambako amekuwa akiniombea kura. Mungu ana njia za ajabu za kufanya mambo.”

Shelukindo alikuwa akirejea fadhila za Lowassa kumwombea kura wakati wa kugombea nafasi ya kamishena wa bunge. Alishinda.

Naye Rostam alitafutwa kwa simu bila kupatikana. Hatimaye alipelekewa swali kwa njia ya sms.

Swali: Kuna taarifa kuwa umeahidi kumwezesha Mhe. Edward Lowassa kwa Sh. 8 bilioni katika kile kinachoitwa “mradi wake wa kujisafisha kisiasa.” Je, hii ni kweli? Simu yako haiitiki.

Tofauti na Lowassa aliyesema hataki kusikia “mambo ya kijinga,” Rostam alijibu kwa sms, “Sidhani Lowassa anahitaji mradi wa kumsafisha maana si mchafu,” kauli ambayo haikushangaza kwa kuwa ilitoka kwa swahiba mkuu wa wakati wa jua na mvua.

Rostam aliandika, “Isipokuwa nimetenga pesa kuwasaidia nyie MwanaHALISI mnunue mtambo wa kuchapisha gazeti bila bughdha!”

Hata hivyo, gazeti hili lina uhakika kuwa Rostam hana mtambo wa kuchapa magazeti yake ya Mtanzania, Rai, The African, Bingwa na Dimba. Anayachapia kampuni ya Mwananchi Communications Limited.

Majibu ya Rostam yameelezwa kuwa ya kumfariji swahiba wake kwa msingi mmoja tu; kwamba wameshiriki – kwa njia mbalimbali – katika kutafuta miradi ya kufua umeme, ambayo imeleta kashfa na kumfikisha Lowassa alipo sasa.

Mtoa taarifa amesema kundi la watu watano limekuwa likifanya vikao; lakini ni kikao cha Dar es Salaam cha mwishoni mwa mwaka jana, ambacho kiliweka mkakati wa Lowassa kujitokeza hadharani “kila inapobidi,” kushiriki mikutano na kutolea matamko hoja kadhaa zinazoibuka ili aonekane karibu na wananchi.

Maswali yaliyotumwa kwa wajumbe wengine wa kundi hili ambao simu zao ziliita bila kujibiwa au hazikupatikana, hayakujibiwa.

Wakati hayo yakifanyika, taarifa zinasema baadhi ya wajumbe wa NEC wamejipanga kupeleka hoja katika vikao vya juu kutaka watuhumiwa wote wa ufisadi waenguliwe kwenye nafasi zao za uongozi ndani ya chama.

“Tunakwenda kwenye NEC tukiwa na dhamira moja ya kumuondoa Rostam, Lowassa na Chenge katika vikao vya maamuzi vya chama chetu. Huo ndio mkakati wetu na lazima tuutekeleze ili kukinusuru chama,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa NEC.

Katika minyukano hiyo, vijana ambao wasiokubali kuingia katika mradi wa kumsafisha Lowassa wameanza kusakamwa. Tayari mjumbe wa Baraza Kuu la uongozi la UV-CCM kupitia mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesimamishwa uongozi na baraza la vijana la mkoa huo.

Pamoja na kutuhumiwa kuhujumu kampeni za mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini, Baltida Buriani, Gambo anatuhumiwa
kumweleza mmoja wa watu walio karibu na Lowassa kuwa “hafai kabisa”, akitumia maneno ambayo, kwa kuzingatia maadili, gazeti hili haliwezi kuyachapisha.

Kauli ya Gambo ilipofikishwa kwa mtoto wa Lowassa, Frederick, mtoto huyo alimwandikia Gambo sms ifuatayo: “Gambo unayo haki ya kumchagu mtu yeyote unayemtaka na siyo kumutukana mzee wangu. Hiyo siyo siasa, lakini endelea.”

Ilikuwa 4 Machi 2011, saa 2:14:39 usiku. Gazeti hili limeona mawasiliano hayo.

Uhusiano wa Gambo na wafuasi wa Lowassa ulizidi kuwa mbaya kutokana na kunukuliwa akielezea wajumbe wa baraza la vijana la taifa mjini Dodoma wiki mbili zilizopita kuwa, sababu kubwa iliyofanya CCM kufanya vibaya katika uchaguzi uliopita, “ni chama kukumbatia watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini.”

“Lowassa na Rostam ndio wanakipotezea mvuto CCM. Tusitafute mchawi. Watanzania wanakerwa sana na Richmond na Dowans na lazima CCM iwashughulikie wahusika wote ili kujenga taswira mpya kwa chama chetu,” alieleza.

Source:- Times of Tanzania Blog