UTAFITI mpya wa kampuni ya Ipsos (Synovate) unaonesha kwamba mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli atashinda kwa asilimia 62 dhidi ya asilimia 31 za mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, endapo Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ungefanyika leo.
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti huo iliyotolewa kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mgombea wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira angepata asilimia 0.3 huku asilimia 7 ya wapiga kura wakiwa hawajui watampigia kura mgombea yupi miongoni wa wagombea wote wa urais kwenye uchaguzi ujao.
Akitoa taarifa hiyo, Mwakilishi Mkazi wa Ipsos hapa nchini, Charles Makau, alisema utafiti huo ulifanyika kati ya Septemba tano hadi 22 mwaka huu na umehusisha wananchi 1,836 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara. “Zanzibar haikuhusishwa katika utafiti huo kutokana na sheria zilizopo visiwani humo kuhusu masuala ya utafiti.
Utafiti ulifuata vigezo vyote vya kisayansi ingawa hatusemi kwamba haya ndiyo matokeo yatakayotokea baada ya upigaji kura wa Oktoba 25 mwaka huu,” alisema. Huu ni utafiti wa pili katika kipindi cha wiki moja ambapo taasisi inayoheshimika kwa masuala ya utafiti inatoa matokeo yanayomwonesha Dk Magufuli kuwa mgombea anayeongoza.
Mapema wiki hii, taasisi ya Twaweza ilitoa matokeo yaliyomwonesha mgombea huyo wa CCM akiongoza kwa asilimia 65 dhidi ya asilimia 35 alizopata mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lowassa ambaye pia anawakilisha umoja wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Nchi (Ukawa).
Tofauti kubwa kati ya utafiti uliofanywa na Twaweza na Ipsos, ni kwamba wakati ule wa kampuni hiyo iliyokuwa ikifahamika kwa jina la Synovate huko nyuma ulifanyika kwa njia ya mazungumzo ya ana kwa ana, ule wa Twaweza ulitumia mawasiliano ya simu za mkononi.
Makau alisema utafiti wa Ipsos ulibaini mambo mbalimbali yakiwamo mambo matano yanayowakera zaidi Watanzania. Mambo hayo ni bei kubwa za vyakula, mafuta na gharama kubwa za kuishi, masuala ya afya, chakula na njaa, maji pamoja na elimu.
Katika sifa mahususi za wagombea urais; wananchi walitoa maoni yao yanayoeleza ni nani wanadhani anaweza kutatua kero kuu zinazowakabili. Dk Magufuli ameonekana kuaminika zaidi katika eneo la miundombinu, ambako asilimia 44 ya waliohojiwa walisema wanaamini atafanya mambo makubwa kwenye eneo hilo huku asilimia 26 wakiamini Lowassa anaweza kufanya hivyo.
Lowassa ameonekana kumzidi Dk Magufuli katika eneo la vita dhidi ya rushwa ambapo asilimia 27 ya waliohojiwa walisema mgombea wa Chadema ataweza kupambana na tatizo hilo huku asilimia 26 wakisema Waziri huyo wa Ujenzi ataweza kupambana na tatizo hilo.
Utafiti huo ulihoji pia ni kwa kiasi gani wananchi wanahisi wako karibu na vyama vya siasa; ambako wale waliosema wako karibu na CCM walikuwa asilimia 60, huku asilimia 29 wakisema wako karibu na Chadema, asilimia 3 wakidai kuwa karibu na CUF huku asilimia moja wakisema wako karibu na NCCR-Mageuzi.
Kwa upande wa jinsia, Magufuli ameonekana kukubalika na wanaume kwa asilimia 51 huku Lowassa ikiwa ni asilimia 37 lakini kwa upande wa wanawake, Magufuli anapendwa na asilimia 69 ya waliohojiwa huku asilimia 21 wakiwa wanampenda Lowassa.
Kama ilivyokuwa kwa utafiti wa Twaweza, Lowassa ameonekana kuwa kivutio cha wenye elimu ya juu na wakazi wa mijini, huku Magufuli akionekana kupendwa na wananchi wa vijijini pamoja na watu wenye elimu ya wastani.
Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi hapa nchini, utafiti huu wa Ipsos ndiyo utakuwa wa mwisho kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mnamo Oktoba 25 mwaka huu. Sheria haziruhusu utafiti wa kisiasa kufanyika na kutangazwa katika muda wa ndani ya siku 30 kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.