CCM Zanzibar Yafanya Tathimini yatarajia Kujipatia Ushindi wa Asilimia 60%


Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar    29/09/2015

Chama cha Mapinduzi CCM kimetoa tathmini yake ya mwelekeo wa Kampeni za Uchaguzi mkuu zinazoendelea nchini na kudai kuwa Mgombea wake wa Urais Dkt Ali Mohamed Shein anakubalika kwa zaidi ya Asilimia 60 dhidi ya Wagombea wengine.

Akitoa tathmini hiyo mbele ya Wanahabari Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai amesema hatua hiyo ni ishara ya ushindi mkubwa kwa CCM kuliko chaguzi zote toka kuasisiwa kwa mfumo wa Vyama vingi nchini.

Vuai amesema kuna mambo mengi ambayo yamemfanya Dkt Shein kukubalika kwa Wananchi ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-15 kwa zaidi ya asilimia 90.


Amesema katika kipindi chake cha uongozi mgombea huyo ameimarisha uchumi kutoka asilimia 6.0 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2014 na kuongeza kasi ya maendeleo.

Aidha Vuai amefahamisha kuwa udhaifu mkubwa wa Mgombea wa Chama kikuu cha upinzani ambaye ameshiriki chaguzi mara nne bila kufanikiwa nayo ni miongoni mwa sababu zinazokipa ushindi CCM.