Vijana watano Tanzania kujaribiwa Orlando Pirates

Vijana watano wa kitanzania wanatarajia kuondoka nchini Agosti 29 mwaka huu kwa ajili ya kufanya majaribio katika timu ya Orlando Pirates iliyopo nchini Afrika ya Kusini.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF Jamal Malinzi amesema, walifikia makubaliano kwa vijana hao na mmiliki wa timu hiyo Irvin Khoza baada ya kuongea naye ambapo watafanyiwa majaribio na wakifuzu watakuwa wachezaji wa Klabu hiyo.
Malinzi amesema, kamati ya ufundi ya TFF kwa kushirikiana na mkurugenzi wake imeona vijana hao wanafaa kujiunga na timu hiyo ambapo wanatarajia kuondoka wakiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Salum Madadi.
Malinzi amewataja vijana hao kuwa ni Hassad Juma kutoka Visiwani Zanzibar, Maziku Aman na Issa Abdi wote wakitokea mkoa Dodoma, Kelvin Deogratius ambaye ni mlinda Mlango akitokea mkoani Geita na Athuman Maulid akitokea Kigoma.
Malinzi amesema, zoezi hilo halijaishia hapo na wanaendelea na mazungumzo na vilabu mbalimbali ikiwemo cha nchini Ureno ili kuweza kupata fursa kwa vijana wengine.