Ndugu zangu wana-CCM na Watanzania wenzangu,
Hii ni siku muhimu kwangu na kwa nchi yetu. Leo nimeamua kuwaita ili kuwatangazia rasmi Watanzania wenzangu azma yangu ya kutaka kuomba ridhaa ya chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), niweze kuteuliwa kuwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nasema hii ni siku muhimu kwangu kwa sababu naamini historia yangu itainakili kama ni siku ambayo kwa mara ya pili katika maisha yangu nimejitokeza kuwania kuiongoza nchi yetu kupitia chama chetu. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi hapa nchini nilipojitokeza nikiwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete; wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Tulikwenda pamoja kuchukua fomu ndani ya Chama na baadaye tukafanya mazungumzo ya pamoja na waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati ya wawili sisi basi mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono.
Ningeweza kujitokeza tena mwaka 2005 lakini nikaamua kwa dhati kabisa kumuunga mkono moja kwa moja Rais Jakaya Kikwete. Nikiwa Mwenyekiti wa Kampeni niliwaongoza wenzangu kufanikisha ushindi mkubwa wa mgombea tuliyemuunga mkono na baadaye ushindi mkubwa wa asilimia 80 wa Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi mkuu wa 2005.
Nitaeleza kwa nini nimeamua kujitokeza tena mwaka huu na kwa nini naamini mimi ndiye mtu sahihi wa kuiongoza nchi yetu wakati huu. Mpaka hapa itoshe tu kuwaeleza ni kwa kwa nini naamini leo ni siku muhimu kwangu.
Lakini nasema ni siku muhimu kwa nchi yetu pia. Nasema hivyokwa sababu naamini inajibu wito wa mahitaji ya sasa ya uongozi wa Taifa letu wa kumpata kiongozi imara atakayewaongoza Watanzania kujenga taifa imara. Na hili pia nitalieleza kwa kina.
HALI YA NCHI NA MATARAJIO YA WATU:
Miaka 48 iliyopita katika jiji hili la Arusha, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage alianzisha mchakato wa kujenga taifa huru kiuchumi na kupiga vita maadui umaskini, ujinga na maradhi kwakutumia silaha ya kujitegemea. Leo hii, wakati taifa likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu ujao, hatuna budi kutafakari tulikotoka, tulipo na tunapotaka kwenda ili tuweze kubuni upya mikakati ya kuhitimisha azma aliyo kuwa nayo Mwalimu, ili tujenge taifa huru, lenye utulivu, mshikamano, amani na maendeleo.
Nchi yetu hivi sasa inapita katika kipindi kigumu cha mpito katika maeneo yote makuu ya maisha yetu – katika siasa, katika uchumi na katika maisha ya kijamii.
Kisiasa, tumeshuhudia kuongezeka kwa vuguvugu la mfumo wa vyama vingi ambapo ushindani kati ya vyama vya siasa unazidi kuwa mkali na kwa bahati mbaya kufikia sura ya kuonekana kama vile ni mapambano ya watu binafsi badala ya mapambano ya sera na dira ya kuongoza nchi. Tunashuhudia kuongezeka uhasama binafsi kati ya wanasiasa ndani ya chama kimoja kimoja na pia kati ya wanasiasa wa chama kimoja dhidi ya kingine. Kadiri siku zinavyokwenda, hali inazidi kuzorota na ikiachiwa kuendelea nchi yetu inaweza kujikuta mahali pabaya. Kukua kwa ushindani ni jambo jema linalokomaza na kurutubisha demokrasia yetu na tukiwa na ushindani wenye afya unaweza kuwa chachu ya kuleta mabadiliko mema kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Kinyume chake ushindani unaochukua sura ya chuki binafsi au kukomoana na hata kulipizana visasi si ushindani wenye tija na tunapaswa kuutafutia tiba. Tunahitaji uongozi imara kusimamia kipindi cha mpito kutoka siasa muflisi za aina hii na kuelekea kwenye siasa mpya zinazoimarisha ushindani wenye tija unaojikita katika kushindana katika kuwapatia huduma bora Watanzania.
Kiuchumi, tumeshuhudia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa mapato ya ndani ya Serikali na uimarishaji wa mfumo wa uwajibikaji na ulipaji kodi. Kwa upande mwengine, Serikali ya Rais BenjaminiMkapa na Rais Jakaya Kikwete imefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi asilia ambapo kiwango kikubwa cha gesi asilia kimegunduliwa. Tanzania sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazovutia uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo ambayo inatajwa kwamba inaweza kuja kubadilisha kabisa maisha ya Watanzania. Hata hivyo, kipindi hiki cha mpito kuelekea ujenzi wa uchumi wa kisasa kimeshuhudia kuongezeka kwa hofu na wasiwasi miongoni mwa wananchi kwamba hawatonufaika naukuaji huu wa uchumi na ugunduzi wa utajiri mkubwa wa gesi asilia. Kwa upande mwingine, vijana wanataka kuona ukuaji wa uchumi na ugunduzi wa utajiri huo unakwenda sambamba na uzalishaji wa ajira zenye maana ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha yao. Niliwahi kusema kwamba tatizo la ukosefu wa ajira likiachiwa bila ya kutafutiwa ufumbuzi imara ni bomu linalosubiri kulipuka. Vijana wasio na ajira hupoteza matumaini na ni rahisi kughilibiwa kuingiza nchi katika machafuko.Tunahitaji uongozi imara kuweza kuikabili hali hiyo na kuitafutia suluhisho maridhawa.
Kijamii, kipindi cha karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya tabia miongoni mwa raia katika hali ambayo haijawahi kuwa sehemu ya utamaduni wa Watanzania. Kumekuwa na ongezeko la kutisha la matukio ya uhalifu linalokwenda sambamba na wananchi kuonyesha wanapoteza imani na taasisi zinazosimamia sheria na usalama na kuamua kujichukulia sheria mikononi mwao. Kumeripotiwa matukio mengi yakiwemo ya kuvamiwa vituo vya polisi, askari kupigwa na kuporwa silaha, matumizi makubwa ya nguvu katika utatuzi wa migogoro mbalimbali hasa ile ya kijamii, mathalani migogoro ya wakulima na wafugaji, mivutano ya kidini na pia mivutano baina ya viongozi wa dini wenyewe kwa wenyewe na baina ya viongozi wa dini na wale wa Serikali. Matokeo yakemshikamano wa taifa nao unaingia majaribuni. Mara nyingine wananchi wanatuuliza viongozi iwapo hii ndiyo nchi tuliyoachiwa na waasisi wetu. Tunahitaji uongozi imara wa kukabiliana na changamoto hizi na kurudisha mshikamano wa taifa letu na watu wake.
WATANZANIA WANATAKA MABADILIKO:
Ndugu zangu, mnaweza kujiuliza kwa nini nimeyaeleza yote hayo na yana mahusiano gani na dhamira yangu ya kutangaza nia ya kutaka kuiongoza nchi yetu kupitia CCM?
Nimeyaeleza haya kwa sababu haya na matukio mengine yanayoendelea nchini yamepelekea Watanzania kutaka mabadiliko. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowawezesha kuzishinda changamoto hizi na kuwaongoza kujenga Taifa imara ambalo kila mwananchi wake anaishi akiwa na uhakika wa mahitaji yake muhimu na papo hapo akijiridhisha kwamba leo yake ni bora kuliko jana yake, na kesho yake itakuwa bora zaidi kuliko leo yake. Kwa maneno mengine, Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayowapa uongozi imara unaoweza kuwaongoza kujenga taifaimara. Hii ndio Safari ya Matumaini.
Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), na watangulizi wake, TANU na ASP, kimepata bahati ya kuungwa mkono na Watanzania tokea enzi za kupigania uhuru, wakati wa Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar, na pia miaka yote tokea Uhuru, Mapinduzi na hatimaye Muungano wetu. Watanzania hawajawahi kushuhudia chama kingine kikiongoza Serikali zetu zaidi ya CCM. Wamekiamini na wanaendelea kukiamini. Hata katika yale majimbo machache ya nchi yetu ambayo hatukufanya vizuri katika uchaguzi, ukiangalia kwa undani utaona si kwamba watu wa maeneo hayo wana matatizo na CCM kama Chama bali wana matatizo na baadhi ya viongozi ambao walishindwa kukiwakilisha vyema Chama na kutambua matakwa ya wananchi hao.
Mimi naamini kwamba hata katika kipindi hiki ambapo Watanzania wanaonekana kutaka mabadiliko bado wanaendelea kuamini kwamba watayapata mabadiliko hayo ndani ya CCM. Lakini kama alivyotupa wasia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini, Watanzania wasipoyapata mabadiliko hayo ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Mimi naamini kwamba CCM tunao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka. Tuwape imani na imani hiyo iwe ni ya dhati na ya ukweli kwamba CCM inao uwezo wa kuwapa uongozi imara wanaouhitaji kwa ajili ya kujenga taifa imara.
Vyama vya siasa vinajumuisha watu na vinaongozwa na watu. Moja ya hulka ya binadamu ni kubadilika kulingana na mahitaji ya mazingira anayoishi. Kwa maneno mengine, binadamu ni ‘dynamic’. Kwa sababu hiyo basi, hata vyama vya siasa vinapaswa kuwa ‘dynamic’. CCM haijapata kuwa na upungufu wa sifa ya ‘dynamism’. Kwa zaidi ya miongo mitano sasa, CCM (na kabla yake TANU na ASP) iliweza kubadili dira na mwelekeo wake ili kwenda sambamba na mahitaji ya Watanzania ya wakati husika. Ndiyo maana tumepita katika vipindi tofauti vya mpito kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto nyingi zilizotukabili. Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani licha ya kubadili mfumo wetu wa siasa kutoka ule wa chama kimoja kuja vyama vingi; licha ya kubadili mwelekeo wa uchumi wetu kutoka ule wa dola kumiliki njia zote kuu za uchumi