Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mrimia Mchomvu (aliyesimama), akisisitiza jambo kwa Wafanyakazi wapya wa Wizara hiyo (hawapo pichani), wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi uliofanyika Jumatatu - Machi 23, 2015, katika Ukumbi wa Elimu ya Watu Wazima – Dar es Salaam. Mkurugenzi Mchomvu alifungua rasmi mafunzo hayo kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara husika, Mhandisi Ngosi Mwihava.
Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mrimia Mchomvu (aliyesimama), akisisitiza jambo kwa Washiriki wa Mafunzo Elekezi kutoka Wizara hiyo (hawapo pichani). Kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi – Sehemu ya Rasilimaliwatu, Lusius Mwenda akifuatiwa na Afisa Utumishi Mwandamizi, Joan Ndibalema. Mkurugenzi Mchomvu alifungua Mafunzo hayo Jumatatu – Machi 23, 2015 kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara husika, Mhandisi Ngosi Mwihava.
Washiriki wa Mafunzo Elekezi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara hiyo, Mrimia Mchomvu (Mstari wa mbele – Katikati). Kulia kwa Mkurugenzi ni Mkufunzi wa Mafunzo hayo kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma akifuatiwa na Mkurugenzi Msaidizi – Sehemu ya Rasilimaliwatu kutoka Wizarani, Lusius Mwenda. Kushoto kwa Mkurugenzi Mchomvu ni Mkufunzi wa Mafunzo kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma, Mariam Kuhenga. Wa kwanza – Kulia (mwenye Koti Nyeusi) ni Ofisa Utumishi Mwandamizi kutoka Wizarani, Joan Ndibalema.
Mmojawapo wa Washiriki wa Mafunzo Elekezi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Ester Njiwa (aliyesimama), akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Washiriki wenzake kwa Uongozi wa Wizara husika, kwa kuandaa mafunzo hayo. Mafunzo hayo ya siku tano (5), yalifunguliwa rasmi Jumatatu – Machi 23, 2015 na Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi, Mrimia Mchomvu kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Ngosi Mwihava.
Washiriki wa Mafunzo Elekezi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wakimsikiliza Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi, Mrimia Mchomvu (aliyesimama), wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo uliofanyika Jumatatu – Machi 23, 2015, katika Ukumbi wa Elimu ya Watu Wazima jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Rasilimaliwatu – Wizara ya Nishati na Madini, Lusius Mwenda (aliyesimama), akizungumza na Wafanyakazi wapya wa Wizara hiyo (hawapo pichani), wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi Jumatatu Machi 23, 2015 katika Ukumbi wa Elimu ya Watu Wazima – Dar es Salaam.
Sehemu ya washiriki wa Mafunzo Elekezi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, wakimsikiliza Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi, Mrimia Mchomvu (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mafunzo husika uliofanyika Jumatatu – Machi 23, 2015, katika Ukumbi wa Elimu ya Watu Wazima – Dar es Salaam. Mafunzo hayo yatahitimishwa Ijumaa – Machi 27, 2015.
Meza Kuu; Kutoka Kushoto ni Waratibu na Wakufunzi wa Mafunzo Elekezi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma, Mariam Kahanga na Dorah Nestory; Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mrimia Mchomvu; Mkurugenzi Msaidizi – Sehemu ya Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Lusius Mwenda na Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Wizara hiyo, Joan Ndibalema.
Na Veronica Simba
Wafanyakazi wapya wa Wizara ya Nishati na Madini wametakiwa kuwa wabunifu wa vyanzo mbalimbali vya mapato sambamba na kuzitafutia suluhu changamoto mbalimbali zinazoikabili Wizara hiyo ili kutekeleza kikamilifu Mpango wa Taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na kuiletea nchi maendeleo.
Pia, wametakiwa kuwa waaminifu na waadilifu katika kutumia rasilimali za Ofisi, pamoja na kudumisha amani na umoja wakati wote ndani na nje ya Ofisi.
Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara, Mrimia Mchomvu aliyasema hayo mapema Wiki hii jijini Dar es Salaam, wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Wafanyakazi hao walioajiriwa hivi karibuni na Wizara husika.
“Tumepewa dhamana ya kuwatumikia Watanzania hivyo tuwajibke ili kufikia viwango vinavyotarajiwa na pia tuweke mikakati thabiti ambayo itasaidia kuongeza pato la Taifa na kutumia rasilimali tunazozisimamia kwa manufaa ya umma wa Watanzania kwa maendeleo ya Taifa,” alisisitiza Mchomvu.
Mkurugenzi Mchomvu, ambaye alifungua Mafunzo hayo kwa niaba ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Mhandisi Ngosi Mwihava alifafanua kuwa, Wafanyakazi ndiyo watekelezaji wa Mpango wa BRN hivyo kila mmoja anatakiwa kuwajibika katika eneo lake na kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa letu ambalo ni changa.
“Mkumbuke kwamba, Wizara yetu inatekeleza Mpango wa Taifa wa Matokeo Makubwa Sasa, ambao matokeo yake yanalenga kuiondoa nchi katika umaskini na kuwa nchi ya kipato cha kati,” alisisitiza.
Akizungumzia suala la upimaji wa utendaji kazi kwa Wafanyakazi, Mkurugenzi Mchomvu alisema kuwa Serikali imeweka Mfumo makini na wazi wa upimaji wa utendaji kazi na mapitio (OPRAS) kwa kila mfanyakazi ambapo utendaji kazi utapimwa kwa uhodari wa kufikia malengo yanayopimika.
Aidha, Mchomvu alizitaja changamoto zinazoikabili Wizara hiyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuongeza uendelezaji na usimamaizi endelevu wa rasilimali za Nishati kwa maendeleo ya Taifa pamoja na kuboresha uendelezaji na usimamaizi endelevu wa sekta ya Madini kwa manufaa ya Taifa.
Nyingine ni uendelezaji wa sekta ndogo ya uchimbaji mdogo wa Madini, kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji wa umeme na kudhibiti upotevu wa umeme wakati wa kusafirisha na kutumia umeme.
“Mchango wenu unahitajika sana katika kuondoa changamoto nilizozitaja. Hatutarajii kupata malalamiko ya utendaji usioridhisha kutoka kwa wateja tunaowahudumia,” alisisitiza Mchomvu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Lusius Mwenda, aliwaasa Waajiriwa hao wapya wa Wizara kutumia elimu na uzoefu walionao katika masuala ya utendaji na uwajibikaji katika utumishi wa umma.
“Ni matumaini yangu kwamba baada ya mafunzo haya, kila mmoja kwa nafasi yake ataweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi unaotarajiwa,” alisisitiza Mwenda.
Mafunzo Elekezi kwa Waajiriwa wapya wa Wizara ya Nishati na Madini, yatahitimishwa Ijumaa, Machi 27 mwaka huu. Waajiriwa hao ni katika Kada za Usimamizi wa Fedha, Mazingira, Uhandisi Migodi, Uhandisi Nishati, Ufundi Sanifu wa Migodi, Afisa Elimu na Wakufunzi.
Kada nyingine ni Maafisa Habari, Maafisa Sheria, Watakwimu, Wakutubi, Wachambuzi Mifumo ya Kompyuta na Maafisa Biashara.