Akitangaza kujiunzulu mbele ya waandishi wa habari mapema leo Jumamosi Januari 24, 2015

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na madini, Prof. Sospeter Muhongo ametangaza kujiuzulu Wadhifa wake wa Uwaziri Katika mkutano wake wa waandishi wa habari aliouitisha hii leo. Profesa Muhongo ametangaza hatua hiyo leo asubuni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam.

Akiongea na Waandishi wa Habari, Prof. Muhongo amezidi kusisitiza kuwa yeye hakuhusika na chochote kile katika sakata hilo lakini baada ya kutafakari sana akagundua kwamba, katika sakata hilo amenyooshewa kidole yeye kama Profesa Muhongo na ni kwa sababu hiyo ameamua kujiuzulu kwa kuzitaja sababu mbili kuwa ni:-

-Ana matumaini kuwa kuachia kwake ngazi, mjadala wa ‘escrow’ utakuwa umefikia tamati.
-Anafanya hivyo ili kukiweka safi Chama Cha Mapinduzi ambacho kimekuwa kinanyooshewa kidole.

Amesema kwa namna moja ama nyingine, sakata hilo si tu kuwa limekuwa likikigharimu Chama bali pia baada ya kutafakari aliwasiliana na mkuu wake wa kazi, Rais Jakaya Kikwete na familia yake na watu wake wa karibu kuwataarifu kuwa anajiuzulu.

Amesema akiwa katika nafasi hiyo, aliweza kufanya mengi ikiwa ni pamoja na kuwapeleka vijana wengi nje kusomea masuala ya gesi, nishati na sayansi kwa ujumla kwani ili Taifa liendelee, linahitaji kuwa na wataalamu katika sekta hiyo muhimu.

Waziri huyo mtaalamu wa miamba, amejiuzulu kufuatia shinikizo la muda mrefu la kumtaka afanye hivyo au awajibishwe, kufuatia mapendekezo ya bunge lililopita, lililoiagiza Serikali kuchukua hatua dhidi ya viongozi wote na watendaji waliohusika na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow iliyobainisha kiasi cha fedha bilioni 302 kuchotwa BOT zilipokuwa zikihifadhiwa.

Mwishoni mwa mwaka jana, 2014, Bunge la Tanzania lilitoka na maazimio ya kutaka kuwajibishwa kwa mawaziri Profesa Sospeter Muhongo, Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema, kutokana na sakata la uchotaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT) kwa kutaka mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao. Mbali na hao, yumo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Profesa Muhongo anakuwa ni kigogo wa nne kufuata mkumbo baada ya Waziri Profesa Anna Tibaijuka kufukuzwa nafasi yake na Rais, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema kujiuzulu mwenyewe, huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi akisimamishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuvunjwa.

Katika hotuba ya mwisho ya Rais Jakaya Kikwete, siku alipotengua uwaziri wa Profesa Anna Tibaijuka alisema amemeweka kiporo Profesa sospeter Muhongo wakati uchunguzi zaidi wa kashfa hiyo ukifanywa.