Mali haina wagonjwa wapya wa Ebola


Waziri wa Afya wa Mali amesema nchi hiyo kwa sasa haina maambukizi ya virusi vya Ebola baada ya siku 42 za kutokuwa na wagonjwa wapya walioambukizwa virusi vya ugonjwa huo .
"Natangaza siku hii, mwisho wa ugonjwa wa virusi vya Ebola nchini Mali," amesema Ousmane Kone.Mtu wa mwisho kuambukizwa Ebola nchini Mali alipona na kuruhusiwa kutoka hospitali mapema mwezi Desemba.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa nchi tatu za Afrika magharibi zilizokuwa zimeathirika zaidi zote zimeshihudia kupungua kwa wagonjwa wapya wa Ebola.
Sierra Leone na Guinea zote zimekuwa na jumla ya chini kabisa ya wagonjwa waliothibitika kila wiki kuambukizwa virusi vya Ebola tangu mwezi Agosti, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zilizotolewa Alhamisi.
Liberia, ambayo haikuripoti wagonjwa wapya kwa muda wa siku mbili wiki iliyopita, ilikuwa na idadi ya chini kabisa kwa wiki ya mambukizi ya Ebola tangu mwezi Juni.
Idadi ya watu waliokufa kutoka na virusi vya Ebola imefikia watu 8,429, huku 21,296 wakiwa wameambukizwa.
Mali iliandikisha mgonjwa wa kwanza wa Ebola mwezi Oktoba, wakati mtoto wa miaka miwili kutoka Guinea alipougua na kufa.
Katika kipindi cha hali mbaya kabisa ya ugonjwa wa Ebola nchini humo watu 300 waliwekwa chini ya uchunguzi kuhusiana na maambukizi ya virusi vya Ebola.
Lakini nchi hiyo kwa sasa imeepukana na ugonjwa huo, amesema Ibrahima Soce Fall, mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Mali kuhusu Ebola (UMEER).
Ugonjwa wa Ebola unachukua siku 21 tangu mtu kuambukizwa hadi kujitokeza kwa dalili za ugonjwa huu na nchi ili kutangaza kuwa zimeondokana na maambukizi ya ugonjwa Ebola lazima zisiwe na wagonjwa wapya kwa vipindi viwili vya matazamio yaani siku 42.