Bunge la EALA lakumbwa na mgogoro
Bunge
la jumuiya ya Afrika mashariki huenda likafungwa iwapo baadhi ya
viongozi wakuu wa Afrika mashariki hawataingilia kati kufuatia migogoro
ya takriban miezi sita sasa inayolikumba.
Hali hiyo inatokana na
kwamba mataifa yaliowachagua viongozi hao kama wawakilishi wake hayana
uwezo wa kuwaadhibu wabunge hao kulingana na Gazeti la jumamosi la The
Citizen nchini Tanzania.Bunge la Tanzania limekiri kwamba halina uwezo wa kuwasimamisha kazi wawakilishi wake katika bunge hilo ,licha ya kwamba wanaendelea kuzozana.
Hatua hiyo inajiri baada ya chama cha FDC nchini Uganda kulitaka bunge la nchi hiyo kuwafuta kazi wawakilishi wake kwa kuwa wabunge hao hawatekelezi wajibu wao.
Kulingana na The Citizen, katika wiki za hivi majuzi ,wanachama wa bunge hilo wameshindwa kufanya kazi zao mjini Kigali na baadaye Nairobi kufuatia mvutano kuhusu madai ya utovu wa nidhamu dhidi ya mwakilishi mmoja kutoka Tanzania ambaye wabunge wanataka aondolewe.
Wanaharakati katika eneo la Afrika mashariki wamelalamika kwamba mgogoro huo unazuia maendeleo ya eneo hili.