Ubaguzi wa rangi:Gyan alalama


Nahodha wa kikosi cha Ghana Asamoah Gyan
Mshambuliaji wa timu ya Ghana anayeichezea kilabu ya Al Ains Asamoah Gyan amemshtumu mchezaji wa timu ya Al Hilal Mihai Pintilii kwa kutoa matamshi ya ubaguzi wa rangi wakati wa mechi ya raundi ya pili ya nusu fainali za kilabu bingwa barani Asia siku ya jumanne.
Kisa hicho kilitokea baada ya Gyan kupewa kadi nyekundu baada ya kumchezea visivyo Salem Al-Dawsari ikiwa zimesalia dakika 20 kwa mechi hiyo kukamilika.
Pintilii ambaye ni raia wa Romania,alimkaribia Gyan ili kutoa hasira zake hatua iliosababisha mvutano kati ya wachezaji kutoka pande zote mbili.
''Pintilii alinitolea matamshi machafu'',alisema nahodha huyo wa timu ya Ghana.Mchezaji huyo hana haki kuniambia yale aliyoniambia.Aliniambia maneno yalionikasirisha''Alisema Gyan.''Anajua kile alichoniambia,unaweza kumuuliza'', aliongezea.
Mshambuliaji huyo aliweka ujumbe wake katika mtandao wa twitter siku ya jumatano akisema kuwa mchezaji huyo alimtolea matamshi ya ubaguzi.
Wakati wa tukio hilo mechi hiyo ilikuwa inaendelea huku timu zote zikiwa zimejifungia bao moja.