Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana kuhusu fainali za mashindano ya Urembo ya Redd’s Miss Tanzania 2014 yatakayofanyika jumamosi. Kushoto ni mwakilishi wa Marie Stopes, Anna Shanalingigwa na meneja wa Redd’s, Vicky Kimario. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Baada ya ubishi wa kisheria mahakamani, sasa mashindano ya ulimbwende ya Miss Tanzania mwaka 2014 yatafanyika Jumamosi kama ilivyopangwa na mshindi atazawadiwa Sh18 milioni.
Lino International Agency ambao ndio waandaaji wa mashindano hayo kupitia mkurugenzi wake, Hashim Lundenga walieleza jana kuwa wameshinda pingamizi la kukataa zuio la mashindano hayo kufanyika na Ukumbi wa Mlimani City utawaka moto Jumamosi ambako mshindi wa pili ataondoka na kitita cha Sh6 milioni na yule wa tatu atazawadiwa Sh4.2 milioni.
Lundenga alisema mshindi wa nne atapata Sh3.2 milioni, wa tano Sh2.2 milioni na washindi wa sita hadi 15, kila mmoja ataondoka na kitita cha Sh1.2 milioni na watakaosalia watapewa kifuta jasho cha Sh700,000 kila mmoja.
Awali, kulikuwa na sintofahamu kuhusu kufanyika kwa mashindano hayo mwaka huu baada ya mmoja wa waanzilishi wa mashindano hayo, Prashant Patel kuweka zuio kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu la kufanyika mashindano hayo.
Hata hivyo, juzi hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Frank Moshi aliruhusu mashindano hayo yafanyike kama lilivyopangwa baada ya kusikiliza maombi ya Patel ya kuomba zuio la mashindano hayo na pingamizi la awali la Lundenga, aliyekuwa akilipinga zuio hilo.
Hakimu Moshi alisema baada ya kusikiliza hoja hizo za pande zote mbili aliona maombi mengine ya Patel yanaweza kuendelea mahakamani hapo, lakini lile la kuzuia mashindano ya Miss Tanzania halina msingi.
Alisema hakimu huyo kuwa kwa sababu hilo linaweza kuleta athari kwa wadhamini, watu waliotegemea kupata manufaa kutokana na mashindano hayo kwa namna moja ama nyingine kwa kutofahamu kama kulikuwapo na mgogoro.
“Kama mashindano yakiendelea, madai bado yatakuwapo palepale na hayawezi kuathiri kesi ya msingi, hivyo hakuna sababu za msingi za kuyazuia mashindano hayo,” alisema Hakimu Moshi.
Alisisitiza kuwa kesi ya msingi itaendelea kusikilizwa Oktoba 21 mahakamani hapo.
Juzi asubuhi, mahakama hiyo ililisikiliza pingamizi la awali lililowasilishwa mahakamani hapo na Lundenga kupitia wakili wake, Audax Kahendaguza ambapo walikuwa wakipinga maombi ya Patel ya kuomba zuio la mashindano hayo ya Miss Tanzania.
Katika pingamizi hilo la awali la Lundenga alikuwa akidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri zilizoombwa na Patel, hati ya kiapo kuunga mkono maombi hayo kina upungufu na maombi yake yaliletwa kabla ya muda.
Baada ya kulisikiliza pingamizi hilo la awali, hakimu alikubaliana na Patel kupitia wakili wake, Benjamin Mwakagamba kwamba mahakama hiyo inayo mamlaka ya kusikiliza maombi hayo ya zuio la mashindano hayo na kwamba yameletwa chini ya vifungu vya sheria vinavyostahili.