Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi ametoa onyo kali dhidi ya maandamano "yasiyo halali" Hong Kong.
Akiwa katika ziara nchini Marekani, Bwana Wang pia alionya kuwa suala la Hong Kong linahusu "mambo ya ndani" ya China
Waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, ameitaka Hong Kong kujizuia na matumizi ya nguvu wakati wa kushughulikia maandamano hayo.
Mapema, waandamanaji wanafunzi waliokasirishwa na China kuwateua wagombea wa uchaguzi wa mwaka 2017 waliapa kuendelea na maandamano iwapo kiongozi wa Hong kong, CY Leung hatajiuzulu.
Wamesema waandamanaji wataanza kukalia majengo ya serikali kama Bwana Leung hatajiuzulu ifikapo Alhamisi.
Waandamanaji walikusanyika usiku kucha nje ya ofisi ya Bwana Leung, huku polisi 200 wakiwa katika eneo hilo.
Bwana Wang, afisa mwandamizi wa China wa ngazi ya juu akizungumzia waziwazi suala hili, alisema: "Masuala ya Hong Kong ni masuala ya ndani ya China. Nchi zote lazima ziheshimu uhuru wa China kujiamulia mambo yake yenyewe. Kwa nchi yoyote, kwa jamii yoyote, hakuna atakayeruhusu vitendo vilivyo kinyume cha sheria vinavyokuika utulivu wa umma."
Hata hivyo, alisema: "Tunaamini kuwa Utawala maalum wa serikali ya jimbo la Hong Kong ina uwezo wa kushughulikia hali hii kwa mujibu wa sheria."
Bwana Kerry amesema Marekani inaunga mkono madhila ya jumla huko Hong Kong, akisema: "Tuna matumaini makubwa kwamba mamlaka ya Hong Kong itajizuia kutumia nguvu na kuheshimu haki ya waandamanaji kueleza mawazo yao kwa amani."