Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akiandaa nyaraka za ushahidi
dhidi ya viongozi waliofukuzwa kwenye chama hicho juzi, kabla ya
kuzungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Kulia ni
Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu. Picha na Fidelis Felix
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imewafukuza uanachama, aliyekuwa
Mwenyekiti wa chama hicho, Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na aliyekuwa
Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo.
“Tumewavua uanachama kutokana na makosa ya kuandaa
waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013,” alisema Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa mbele ya waandishi wa habari.
Wakati hayo yakifanyika, imeelezwa kuwa aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe ataendelea na uanachama na ubunge
kwa sababu ya mahakama, siyo kwa matakwa ya chama hicho.
Zitto ambaye alitajwa kuwa mhusika mkuu katika
waraka huo amefungua kesi akiomba Mahakama Kuu izuie uanachama wake
kujadiliwa hadi rufani yake itakaposikilizwa na Baraza Kuu la chama.
Hatima ya maombi hayo itajulikana leo.
Maamuzi ya kikao
Akitangaza uamuzi wa kikao cha dharura cha Kamati
Kuu kilichokutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam jana, Dk Slaa
alisema, “Kuhusu Zitto Kamati Kuu haikujadili wala kuamua juu ya
mashtaka dhidi yake.”
Huku akiyataja makosa 11 ya Zitto, Mwigamba na Dk
Kitila yaliyotokana na waraka huo, Dk Slaa alisema, “Baada ya kumhoji Dk
Mkumbo alikiri wazi kuwa Zitto alikuwa akiujua waraka huu ambao
ulilenga kukiuka chama, kutengeneza tuhuma dhidi yangu na Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe.”
Katika mkutano huo Mwanasheria Mkuu wa chama
hicho, Tundu Lissu alisema Zitto ataendelea kuwa mwanachama wa Chadema
na mbunge kwa sababu ya mahakama na siyo matakwa ya Chadema.
Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Mwigamba na Dk Kitila, Novemba 22 mwaka jana walivuliwa nyadhifa zao na
Kamati Kuu baada ya kukamatwa kwa waraka huo.
Waraka huo ulioandaliwa na Mwigamba na Dk Kitila,
uliolenga kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi wakati wa uchaguzi
mkuu wa ndani wa chama hicho, huku Zitto akipendekezwa kuwania nafasi ya
uenyekiti.
Utetezi wa watuhumiwa
Katika ufafanuzi wake kuhusu utetezi wa
watuhumiwa, Dk Slaa alisema, “Dk Kitila pekee, ndiye alikuja kuhojiwa na
Kamati Kuu iliyokutana Januari 3 hadi 4 na kwamba alikubali kuandaa
waraka lakini alikataa kwa kuwa ulikiuka katiba na kanuni za chama. Pia
alikataa kumtaja kwa jina mwandishi mwingine wa waraka huo anayetajwa
kwa jina la M2.”
Alisema wakati wa mahojiano hayo, Dk Kitila alikiri wazi kuwa
yeye na waandishi wenzake walimpa taarifa Zitto kuhusu mkakati huo na
kwamba alikuwa anaufahamu. Hata hivyo, katika kikao cha Kamati Kuu
kilichofanyika Novemba 22, mwaka jana, Zitto alisema kuwa alikuwa hajui
chochote kuhusu waraka huo.
Alisema Dk Kitila alikataa kujadili hoja aliyoiibua kwamba Chadema kimebadili katiba yake na kuondoa ukomo wa uongozi.
“Pia Dk Kitila alieleza kuwa chama kinatumia
fedha ovyo, kikao kilitoa taarifa za fedha zilizojadiliwa katika vikao
vilivyopita wakati yeye na Zitto wakiwa wajumbe, alionyeshwa michango ya
fedha ya Jaffer Sabodo na ya watu wengine, ununuzi wa vifaa vya chama
na jinsi mwenyekiti wa chama asivyohusika kuidhinisha matumizi ya
fedha,” alisema.
Uamuzi wa Kamati Kuu
Alisema baada ya kumsikiliza Dk Kitila, Kamati Kuu
imebaini kuwa mkakati huo haukulenga kumfanya Zitto kuwa mwenyekiti
pekee, bali ulikuwa na malengo makubwa ya kukibomoa chama hicho.
“Ulilenga kukichafua chama, viongozi wake na
kutumia tuhuma za uongo za ufisadi kwa sababu walifahamu kuwa chama
chenye viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi kuaminiwa na
wananchi,” alisema Dk Slaa.
Lissu amlipua Zitto
Kwa upande wake Lissu alisema Zitto alikihujumu
chama hicho na kushiriki kujitoa kwa wagombea wake wa ubunge katika
majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini, Singida Mjini na kuwa
mwaka 2006, alipewa magari mawili na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM).
Akijibu madai hayo, Zitto alisema hizo ni tuhuma
mpya kama viongozi wa Chadema wanataka azijibu wamwandikie badala ya
kupayuka kama kasuku.
Mwigamba, Dk Kitila wajibu
Kwa upande wake Dk Kitila Mkumbo alisema, “Sina
pingamizi lolote kuhusiana na hatua ya kuvuliwa uanachama na kwa sasa
natafakari hatima yangu kisiasa. Sipingi uamuzi nilijitetea lakini
hawajaridhika na majibu yangu. Mimi ni muumini wa vyama vingi vya siasa,
naamini iko siku nitajiunga na chama chochote, lakini ninachokifanya
sasa ni kutafakari tu.”
Naye Mwigamba alisema hajashangazwa na kitendo cha
kuvuliwa uanachama kwa kuwa tangu siku nyingi alijua uamuzi huo
ungefanywa dhidi yake.
“Acha waendelee na chama chao, nitaendelea kuamini kilichoandikwa kwenye waraka, tulichokifanya katika waraka ule kililenga kukisaidia chama.
MWANANCHI
“Acha waendelee na chama chao, nitaendelea kuamini kilichoandikwa kwenye waraka, tulichokifanya katika waraka ule kililenga kukisaidia chama.
MWANANCHI