Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kuifanyia utafiti wa kina na hatimae
kusaidia kugharamia ujenzi wa kudumu wa Bara bara itokayo Unguja Ukuu
kuelekea Uzi Kisiwani yenye urefu unaokadiriwa kufikia Kilomita Mbili
Nukta Sita ambayo hivi sasa bado iko katika kiwango cha mawe matupu.
Ombi
hilo limetolewa na Wananchi wa Vijiji vya Unzi na N’ambwa mbele ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara
fupi ndani ya Jimbo la Koani kuangalia maendeleo na matatizo
yanayowakabili wananchi wa Jimbo hilo liliomo ndani ya Wilaya ya Kati
Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi
Seif Ali Iddi akipata wasaa wa kuikagua kwa kina Bara bara hiyo ya
Unguja Ukuu hadi uzi ambapo Wananachi wa Vijiji hivyo chini ya
Mwenyekiti wao wa Ujenzi wa Bara bara hiyo Mzee Shaya Mohd hawakuchelea
kumuelezea kadhia wanayopambana nayo wanapovuka sehemu hiyo hasa
wakati wa maji Makuu.
Mzee
Shaya Mohd alifahamisha kwamba Wananchi wa Vijiji hivyo wamefikia hatua
ya kukata tamaa kutokana na kadhia ya maji yanayosababisha kupangua
mfumo wa mawe licha ya juhudi kubwa wanazozichukuwa katika kupanga mawe
hayo katika kila baada ya kipindi kifupi.
Alisema
baadhi ya wananachi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa hasa akina Mama
wajawazito wakati mwengine hulazimika kujifungulia njiani kutokana na
kadhia ya Bara bara hiyo jambo ambalo huleta hatari kwa mazingira ya
mzazi na motto mwenyewe.
“ Bara
bara yetu iliwahi kufanyiwa Utafiti na hatimaye kujazwa mchanga katika
katika Bara bara hii katika miaka ya thamanini lakini kilichojitokeza
mara baada ya kupunguwa kwa kiwango cha maji makuu mchanga wote
uliowekwa umekwenda na maji hayo “. Alifafanua Mzee Shaya Mohd Haji.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu hadi
Uzi - N’gambwa alifafanua kwamba njia pekee ya kukabiliana na
tatizo hilo kulingana na mfumo wa maji ya bahari yanayokata katika eneo
hilo ni kutumiwa kwa saruji,kokoto na mawe kwenye ujenzi wa Bara bara
hiyo ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu katika matumizi yake.
Akielezea
kadhia ya ukosefu wa huduma ya Maji safi na Salama ndani ya Kijiji
cha N’gambwa naye Mzee wa Kijiji hicho Bwana Khatib Mussa alimsikitikia
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Wananchi wa Kiji
hicho wanashindwa kuendelea vyema na harakati zao za kimaisha kutokana
na muda mwingi kuutumia katika kutafuta huduma hiyo.
Mzee
Khatib Mussa alifahamisha kwamba huduma za maji safi ambazo ziliwahi
kufika Kijijini hapo katika miaka michache iliyopita lakini hivi sasa
zimekatika kabisa na kuifanya jamii ya kijiji hicho kuwa katika
mazingira ya hatari kiafya.
Akizungumza na Wananachi hao wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa kwa nyakati
tofauti Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
ameiagiza Wizara ya Mawasiliano na Miundo Mbinu Zanzibar kuiweka katika
Bajeti yake ya Mwaka Ujao Bara bara hiyo ili Serikali ipate fursa ya
kuitengea fedha za ujenzi.
Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi hao wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa
kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuona matatizo
yanayowakabili wananchi wake katika maeneo mbali mbali hapa Nchini
yanapatiwa ufumbuzi wa kina.
“ Kwa
kweli tunataka kuona Vijiji vya Uzi na N’gambwa ndani ya Jimbo la
Koani Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja vinabadilika na kuwa vya
kisasa ili vilingane na vijiji vyengine hapa Nchini “. Alieleza Balozi
Seif.
Katika kuunga mkono juhudi za Wananchi hao wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliahidi kuchangia
Matofali 1,000 pamoja na saruji Mifuko 10 kwa ajili ya kuongeza nguvu za
ujenzi wa Jengo Jipya la Skuli ya Uzi linalotayarishwa kwa ajili ya
wanafunzi watakaoingia Elimu ya Sekondari hapo mwakani.
Balozi Seif pia akaahidi kuzipatia seti moja moja na mipira miwili kwa
kila Timu za Soka za Wanawake wa Vijiji vya Bungi na Kidimni pamoja na
kuitaka Kamati ya Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu Uzi kufanya makisio
ya ujenzi wa Banda la Hifadhi wakati wa kujaa kwa maji liliopo kwenye
jiwe kubwa la Kihistoria kati kati ya Bara bara hiyo.
Naye Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mh. Ramadhan Abdullah
Shaaban akitoa ufafanuzi katika Mkutano wa Hadhara wa Wananachi hao juu
ya tatizo la Maji safi na Salama Uzi na N’gambwa alisema Wizara hiyo
iko katika hatua za mwisho kutafuta Pampu kubwa itakayokuwa suluhu ya
tatizo hilo.
Hata hivyo Waziri Shaaban alifahamisha kwamba katika juhudi za kuisaidia
nguvu Pampu hiyo wataalamu wa Wizara hiyo wanatarajia pia kujenga Tangi
la Maji kati kati ya Vijiji vya Uzi na N’gambwa ambalo litakuja
kusaidia kusambaza kwa uhakika huduma hiyo.
Akisoma Risala ya Wananchi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa Mjumbe wa
Kamati ya Maendeleo ya Vijiji hivyo Ndugu Abdu Mohd Khamis alisema
Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu hadi Uzi tayari umeshagharimu jumla
ya shilingi za Kitanzania Milioni Mia 166,019,000/- hadi sasa.
Ndugu Abu Mohd alisema kati ya fedha hizo Shilingi Milioni 124,633,000
ni nguvu za Wananchi, Shilingi Milioni 25,786,000 zimetolewa na Mbunge
wa Jimbo la Koani na Shilingi Milioni 15,600,000 zikatolewa na
Mwakilishi wa Jimbo hilo la Koani.
Alisema wananchi wa Vijiji hivyo wameishukuru Idara ya Ujenzi wa Bara
bara Zanzibar { UUB } kwa hatuzake za mashirkiano na wananachi hao
yaliyopelekea kwa kiasi kikubwa kuwawezesha kuitumia kwa unafuu Bara
bara hiyo.
Mjumbe huyo wa Kamati ya Maendeleo alisema Vijiji hivyo pia vinakabiliwa
na tatizo la ukosefu wa huduma za Umeme ambalo Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif tayari ameshaiagiza Wizara inayohusika na
masuala ya Umeme kulibeba jukumu hilo kwa kutafuta nguzo 10 na waya zake
ili kuliondosha tatizo hilo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/1/2014.
Baadhi
ya Wananchi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa wadogo kwa wakubwa
wakiendelea na harakati za matengenezo ya barabara yao itokayo Unguja
Ukuu hadi Uzi kila baada ya kupungua kwa kina cha maji.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ujenzi wa Bara bara ya Unguja Ukuu – Uzi Bwana Shaya
Mohd akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif eneo
lenye kupitisha maji mwengi ambayo huleta kadhia kwenye barabara yao.
Balozi
Seif akikagua barabara ya Unguja Ukuu hadi Uzi ambayo iko katika
kiwango cha mawe ambayo inatengenezwa na Wananachi wenyewe.
Moja
ya Visima vichache vilivyomo ndani ya Kijiji cha N’gambwa ambavyo vina
upungufu mkubwa wa maji kiasi kinachochangia kuleta usumbufu wa huduma
hiyo ndani ya Kijiji hicho.
Mzee
Khatib Mussa wa Kijiji cha N’gambwa akimueleza Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif juu ya kadhia ya muda mrefu inayowasumbua ya
ukosefu wa huduma za Maji safi na salama kijijini pao
Katibu
wa Kikindi cha Ushirika cha Hapa Kazi chenye wanachama 48 katika Kijiji
cha Uzi ambae ni Mlemavu Bibi Mwanajuma Harufu Haji akimnon’oneza Kitu
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mara baada ya kuzungumza
na wananachi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa katika Picha ya Pamoja na
wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Uzi mara baada ya kuzungumza na
wananchi wa Vijiji vya Uzi na N’gambwa. Kulia
ya Balozi mwenye kilemba ni Mbunge wa Jimbo la Koani Mh. Amina Andrew
na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Nd. Ramadhan Abdulla Ali.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.