Baadhi
ya shehena za vipodozi zilizokamatwa na jeshi la polisi mkoa wa Iringa
baada ya kushushwa katika roli katika makao makuu makuu ya jeshi mkoa
wa Iringa.
Kamanda
wa Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa ACP Ramadhani Mungi akionyesha
shehena ya vipodozi vilivyokamatwa na jeshi hilo mkoani Iringa katika
makao makuu ya jeshi hilo jana.(picha na Denis Mlowe)
JESHI
la polisi mkoa wa Iringa limefanikiwa kukamata shehena ya vipodozi
vyenye thamani ya mamilioni ya shilingi iliyokuwa inasafirishwa kutoka
nchini Zambia kwenda jijini Dar es Salaam vilivyopigwa marufuku kwa
matumizi ya binadamu.
Shehena
hizo zilikuwa zimebebwa na gari aina ya lori la mafuta lenye namba za
usajili T 247 BHP na tela lenye namba usajili T 598 BMK mali ya World
Oil Ltd ya jijini Dar es Salaam.
Waliokamatwa na shehena hiyo ya vipodozi ni Dereva wa lori Mohamed Sadru(23) na Kassimu Kaifa anayesadikika ndio mwenye mali.
Kamanda
wa jeshi la Polisi mkoa wa Iringa ACP Ramadhani Mungi amethibitisha
kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kusema kuwa walipata taarifa za
kiitelejensia kutoka Tunduma kuwa kuna lori linasafirisha shehena hiyo
kutoka nchini Zambia.
Mungi
alisema walijiweka tayari kulikamata gari hilo kwa kukaa barabara kuu
kuanzia saa moja jioni hadi ilipofika saa kumi alfajiri ndipo gari
lilipofika na kukamatwa.
Anaongeza
kuwa maafisa wa polisi mkoa wa Iringa walijipanga vizuri kuweza
kulikagua gari hilo na waligundua kuna shehena kubwa ya vipodozi
vilivyopigwa marufuku na TFDA na kuwaweka chini ya ulinzi dereva na roli
hilo.
“Cha
kushangaza gari la mafuta kuweza kubeba vipodozi hivi vilivyopigwa
marufuku hivyo tukaamua kuwashirikisha wadau wengine ambao ni TRA, TFDA
na Tanroad kuweza kubaini makosa ambayo watuhumiwa hao wamefanya katika
usafirishaji wa shehena hiyo.” Alisema Mungi
Mungi
alisema uchunguzi wa awali unaonyesha shehena hiyo ina thamani kubwa na
ndio maana watuhumiwa walikuwa wanasafirisha kwa njia ya magendo na
wanaendelea kuchunguza kubaini thamani halisi ya mzigo huo.
Kwa
upande wake Mratibu wa Mamlaka wa Chakula na Dawa (TFDA) mkoa wa
Iringa, Deodata Rukupwa alisema shehena iliyokamatwa asilimia 100 ina
kemikali iliyopigwa marufuku ya Hydroqunone na mamlaka hiyo.
Alisema
vipodozi hivyo vitateketezwa kwa pamoja na jeshi la polisi na gari hilo
kutaifishwa na serikali kutokana na kubeba mzigo wa magendo.
Na Denis Mlowe,Iringa
kwa hisani ya Pamoja blog