Katibu
Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema
chama chake kitaendelea kusimamia misingi ya haki na usawa, ili
kuhakikisha kuwa kila Mzanzibari anapata haki yake inayostahiki.
Maalim
Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo
wakati akihutubia mkutano wa hadhara ya chama hicho uliofanyika viwanja
vya Kinyasini, jimbo la Chaani.
Amesema
Chama hicho kitaendelea kuwa mstari wa mbele kudai mamlaka kamili ya
Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha kuwa Zanzibar inaongozwa kwa misingi
ya haki na usawa, ili wazanzibari waweze kuamua mambo yao wenyewe bila ya kuingiwa na mamlaka nyengine.
Amesifu
umakini wa kamati ya Maridhiano yenye wajumbe sita wakiwemo watatu
kutoka Chama Cha Mapinduzi na watatu kutoka Chama Cha CUF, na kwamba
wajumbe wa kamati hiyo wameonesha uzalendo wa hali ya juu katika
kutekeleza majukumu yao.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maridhiano Mzee Hassan Nassor Moyo,
amebainisha kuwa mambo yanayodaiwa kutolewa katika orodha ya Muungano
sio mageni, kwani yalikuwemo kwenye mamlaka ya Zanzibar kabla ya
kuungana na Tanganyika mwaka 1964.
Ameyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na sarafu, mambo ya nje, pamoja na rasilimali ya mafuta na gesi asilia.
Mzee Moyo amewanasihi Wazanzibari kuepuka chuki, fitna na ubaguzi, na badala yake waungane kupigania maslahi ya nchi yao.
Amepongeza
hatua iliyochukuliwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid
Karume na mwenzake Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ya
kufikia maridhiano ambayo yamewaunganisha Wazanzibari.
Nae
Mjumbe wa Kamati hiyo ya maridhiano Mansoor Yussuf Himid (CCM), amesema
Zanzibar ni ya Wazanzibari wote, na kwamba kila mzanzibari anastahili
kupata haki sawa na mwengine.
Amesema
ataendelea kuungana na Wazanzibari kupigania haki ya Zanzibar ndani ya
Muungano, ili iweze kuendesha mambo yake yenyewe, na kuwashajiisha
vijana kutorudi nyuma katika kupigania haki hiyo.
Akizungumzia
kuhusu rasimu ya pili ya katiba inayotarajiwa kuwasilishwa kesho (leo)
tarehe 30/12/2013 katika viwanja vya Karimjee Dar es Salaam, Mansoor
amesema ikiwa rasimu hiyo haitokidhi angalau wastani wa matakwa ya
Wazanzibari hawatoikubali, na wataikataa kabisa.
“Watu
wa mjini huwa tuna wimbo tunasema ‘supu tayari…’ lakini tunasema ikiwa
supu hii ya Jaji Warioba itapungua chumvi au pilipili manga tutaiongeza,
lakini kama mbaya hailiki tutamuachia mwenyewe supu yake” alidokeza
Mansoor.
Wajumbe
wengine wanaounda kamati hiyo ambao wote walikuwepo mkutanoni na
kuzungumza ni Abubakar Khamis Bakar (CUF), Ismail Jussa Ladhu (CUF),
Eddy Riyami (CCM) na Salim Bimani (CUF).
Katika
Mkutano huo Mhe. Maalim Seif alikabidhi kadi 459 kwa wanachama wapya
walioamua kujiunga cha chama hicho, sambamba na kuweka mawe ya msingi
katika matawi matatu mapya ya CUF ndani ya jimbo la Chaani, pamoja na
kufungua barza ya vijana, iliyoyopewa jina la barza ya Maalim Seif
Sharif Hamad katika kijiji cha Bandamaji Chaani.
Na Hassan Hamad OMKR- Zanzinews