Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif amesema leo kuwa anaunga mkono juhudi za Afghanistan za kutafuta amani na Taliban na kwamba atawasaidia wajumbe kukutana na kamanda mmoja wa zamani wa kundi hilo.
Akizungumza akiwa mjini Kabul baada ya kukutana na Rais wa Afghanistan Hamid Karzai, Sharif amerudia usemi wake kuwa serikali yake ilimwachia kamanda wa zamani Mullah Baradar, ambaye anazingatiwa na Afghanistan kama ni mtu muhimu katika kulileta kundi la Taliban kwenye meza ya mazungumzo.
Ziara hiyo ya siku moja ni ya kwanza kwa Sharif tangu alipochukua uongozi mwezi Mei na inajiri wakati Karzai akiwa katika mzozo wa hadharani na Marekani kuhusiana na mpango muhimu wa usalama unaohusu jukumu la majeshi ya Marekani yatakayosalia Afghanistan baada ya NATO kuondoka mwaka ujao. Sharif pia amekutana na Baraza Kuu la Amani nchini Afghanistan, ambalo linataka kuanzisha mazungumzo na wanamgambo wa Taliban ambao wamekuwa wakipambana na jeshi la NATO linaloongozwa na Marekani tangu mwaka wa 2001.