MAMA na mtoto wakazi wa kijiji cha
Iseche kata ya Mwambani Tarafa ya Kwimba Wilayani Chunyani Mkoani Mbeya
wanatafutwa na jeshi la polisi Mkoani hapa kwa tuhuma za kumuua mume
wake aitwaye ,Silvester Alphonce Chikondo(55)baada ya kushambuliwa kwa
malungu na mke wake kwa kushirikiana na mtoto wake wa kiume.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la
Polisi kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa polisi mkoa wa
Mbeya Mkoani Mbeya ,Diwani Athuman alisema kuwa tukio hilo limetokea
Novemba 12 mwaka huu majira ya saa 2.00 usiku katika kijiji cha Iseche
wilayani hapo.
Kamanda Athuman alisema kuwa marehemu
alikutwa na mauti hayo wakati alipokuwa akitoka kilabuni kunywa pombe
ndipo mama huyo kwa kushirikiana na mwanae wa kiume walipoanza
kumshambulia kwa malungu kwa kile kinachodaiwa wivu wa kimapenzi.
Hata hivyo Kamanda Athuman alisema
kuwa mke wa marehemu na mwanae wa kiume walimshambulia marehemu huyo kwa
kumpiga na malungu kichwani,utosini pamoja na ngumi na mke wake
aliyejulikana kwa jina la Husulinakornel (42) akiwa na mwanae Kondo
Alphonce Chikondo(19)
Akizungumzia mazingira ya tukio hilo
Kamanda Athuman alisema kuwa mbinu iliyotumika ni kumshambulia kwa
kumpiga baada ya kufika nje ya nyumba wakitokea kilabuni kunywa pombe
za kienyeji.
Alisema kuwa chanzo cha ugomvi huo ni
wivu wa kimapenzi kufuatia marehemu kuongea na mwanamke mwingine wakati
wakiwa kilabuni na mkewe walipokuwa wakinywa pombe ndipo mke wa
marehemu alipoingiwa na wivu na kuanza kuleta ugombi wakiwa kilabuni.
Baada ya kipigo hicho kutoka mkewe na mwanae wa kiume marehemu alianguka kisha kufariki dunia papo hapo.
Mama huyo akiwa na mwanae walikimbia
na kukimbilia kusikojullikana mara baada ya kugundua mumewe amefariki
dunia na kwamba mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na kubainika
ubongo kuchanganyika na damu hivyo kusababisha kifo chake.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mbeya kamishna msaidizi wa polisi Diwani Athumani ametoa wito kwa
jamii hasa wanandoa kutatua matatizo kwa njia ya kukaa meza ya
mazungumzo na kujenga hoja badala ya kujichukulia sheria mkononi na
kutumia nguvu kwani ni kinyume cha
sheria na pia kuepusha matatizo yanayoweza kuepukika.
Aidha Kamanda alisema kuwa mtu yeyote
mwenye taarifa juu ya mahali walipo watuhumiwa azitoe katika mamlaka
husika ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake, vinginevyo
wajisalimishe wenyewe.

