Marekani yajitolea kuteketeza silaha za sumu za Syria

Marekani imejitolea kuziteketeza silaha za sumu za Syria. \
Shirika la Kimataifa la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Sumu -
OPCW limesema leo kuwa silaha hizo zitaangamizwa kwa kutumia meli ya Marekani, na kuwa nchi hiyo inatafuta bandari muafaka katika bahari ya Mediterenia ambako shughuli hiyo inaweza kufanyika. 
OPCW imekuwa ikikabiliwa na mbinyo wa kutafuta mpango mbadala wa kuziangamiza gesi za sumu za Syria baada ya Albania kukataa kujiitwika mzigo huo. 
Kampuni 35 zilikuwa zimewasilisha maombi yao kabla ya muda wa mwisho siku ya Ijumaa ya kupewa kandarasi za kibiashara kushiriki katika shughuli ya kuziharibu karibu tani 800 za sumu ambazo ni salama kuteketezwa katika viwanda vya kawaida. 
Lakini tani nyingine 500 za sumu, inaonekana kuwa hatari zaidi kusafirishwa hadi nchi nyingine au kuharibiwa katika viwanda vya kawaida, na hivyo zitateketezwa baharini kwa kutumia meli hiyo ya Marekani.