Marekani inasema kuwa madai ya Kony ni kiini macho tu
Afisa kutoka katika wizara ya mambo ya ndani nchini Marekani, ameambia BBC kuwa waasi kadhaa walishauriana na serikali ya CAR wala sio Kony mwenyewe.
Marekani iliahidi kutoa zawadi ya dola milioni 3.3 kwa mtu yeyote mwenye taarifa ambayo ingepelekea kukamatwa kwa Kony.
Kony alianzisha kundi la waasi la LRA, kaskazini mwa Uganda, zaidi ya miaka 20 iliyopita, na waasi wake wanasifika kwa kuwateka nyara watoto na kuwaingiza katika kundi lao la waasi kama wapiganaji pamoja na kuwa watumwa wa ngono.
Maafisa hao walielezea kuwa Kony amewahi kutumia mbinu zote kama hizi kupumzika, kujikusanya upya na waasi wake na hata kujihami upya na kisha kuanza kuteka nyara, kuua na kusababisha watu kutoroka makwao.
Waasi wa LRA walilazimika kutoroka Uganda mwaka 2005 na tangu hapo wamekuwa wakifanya vurugu katika CAR, Sudan Kusini na katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Nusura Joseph Kony atie saini mkataba wa Amani mwaka 2008 lakini akasisitiza kuwa mahakama ya ICC mwanzo itupilie mbali kibali cha kumkamata , ingawa mahakama hiyo ilikataa kufanya hivyo.
Na BBC/Swahili
