WAKAZI BOTI ZA DAR – ZANZIBAR ZASITISHA HUDUMA, WAKAZI WA MWAMBAO KIWEWE, SERIKALI YATOA TAMKO
WAKAZI wa mikoa iliyoko katika mwambao wa pwani; Dar es Salaam, Lindi, Tanga na Visiwa vya Zanzibar, jana walikumbwa na taharuki kubwa baada ya kuwepo taarifa za uwezekano wa kutokea tetemeko la ardhi chini ya bahari ya Hindi, tsunami.
Habari za tsunami zilisambaa mchana na kuifanya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Bunge kutoa taarifa za tahadhari kwa wananchi.
Hofu iliwakumba zaidi wakazi wa Dar es Salaam ambako ndiko kitovu kikuu cha shughuli za kiuchumi na kibiashara Tanzania na usafiri wa majini kati ya Zanzibar na jiji hilo ulisimamishwa hadi leo kupisha tahadhari hiyo.
Tsunami hiyo ambayo jana iliathiri maeneo mbalimbali ya bara la Asia hasa kisiwa cha Sumatra, Indonesia pia lilitarajiwa kusambaa katika ukanda wa baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Kenya, Somalia na Msumbuji.
Onyo la TMA
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Agnes Kijazi alisema jana kwamba tsunami hiyo ilitarajiwa kuyakumba maeneo hayo kati ya saa 1:00 na saa 3:00 usiku.
Kijazi aliwataka wananchi hasa waishio nyumba zilizo karibu au kando ya bahari kuwa makini akisema lolote linaweza kutokea. Aliwashauri pia wanaotumia bahari kwa usafiri na uvuvi wasiende baharini majira hayo.
Kijazi alisema tsunami hiyo inakuja kwa kasi kubwa ikianzia Indonesia na inaelekea katika Pwani ya Tanzania hivyo kuanzia jana, wananchi ambao wana mazoea ya kukaa pembezoni mwa bahari wametakiwa wasifanye hivyo.
“Tunatoa tahadhari kwa wananchi wote ambao wanatumia usafiri wa majini wasitishe safari zao kuanzia saa 10:00 jioni (leo) jana, kutakuwepo na mawimbi makubwa baharini,” alisema.
Kwa kawaida, tsunami inapotokea husababisha uharibifu mkubwa wa mali na hata vifo kwa binadamu na viumbe hai wengine.
Kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya habari ya kimataifa yakiwemo Reuters na Sky News, tetemeko lililotarajiwa kutikisa Dar es Salaam, lilikuwa la ukubwa wa 6.7 kwa kipimo cha richter na hali ilitarajiwa kuwa mbaya zaidi Lindi ambako tetemeko hilo lilitarajiwa kufikia kipimo cha 9.7 katika kipimo cha ritcher.
Mwaka jana, Japan ilikumbwa tetemeko hilo lenye ukubwa wa kipimo cha 8.9 richter, (ambalo ni dogo ukilinganisha na kipimo cha Lindi) na liliripotiwa kuua mamia ya watu kwa kuangukiwa na nyumba na mafuriko makubwa ya maji yaliyotapakaa kuanzia baharini na kubomoa nyumba, kuzamisha magari, meli na kusababisha moto mkubwa baadhi ya maeneo.
Hali Dar es Salaam
Katika jiji la Dar es Salaam, hali ya taharuki ilikuwa mbaya zaidi mbaya zaidi majira ya jioni ambapo karibu barabar zote za katikati ya jiji zilikuwa na msongamano mkubwa wa magari.
Wananchi wengi walioonekana barabarani baada ya kusitisha shughuli zao mapema kuwahi kurudi nyumbani kupisha tishio hilo.
Kutokana na hali hiyo, kulikuwa na foleni kubwa katika barabara karibu zote kubwa kiasi cha baadhi ya wananchi kuamua kutembea kwa miguu huku barabara zikiwa zimejaa maji.
Hata mawasiliano ya mitando ya simu yalikuwa ya shida kwa muda hasa jioni kati ya saa 10:00 hadi saa 11:00 jioni. Tatizo hilo pia liliongeza hofu kwa wakazi wa jiji hilo.
Katika eneo la Mtongani, Mto Kizinga ambao ni mkondo wa Bahari ya Hindi, ulijaa maji na makazi ya watu kuzingirwa na maji.
Wavuvi na wakaanga samaki katika Soko la samaki Feri, walikuwa wameondoka wote ilipofika saa 12:00 jioni.
Hata maeneo mengi ya fukwe hayakuwa na mtu yeyote huku taarifa za kutokea kwa janga hilo la tsumani zikitawala mazungumzo karibu kila kona ya jiji.
Fukwe nyeupe Tanga
Shughuli za uvuvi pamoja pilika nyingine katika fukwe na sehemu nyingine za Pwani ya Bahari ya Hindi upande wa Mkoa wa Tanga, jana zilisimamishwa baada ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuzuia.
Uzuiaji wa shughuli hizo ulitokana na taarifa za kuwepo kwa tetemeko hilo la tsunami kwenye Pwani ya Bahari ya Hindi.
Maeneo ya pembezoni mwa bahari ambayo huwa na pilikapilika za wavuvi na wachuuzi wengine, jana zilikuwa nyeupe.
Katika eneo la Rascazone ambalo kila siku jioni huwa na waogeleaji wengi wakiwamo watalii, kutoka nchi za nje jana halikuwa na watu na ilielezwa kwamba wameondoka kutokana na hofu
Ofisa wa Sumatra Mkoa wa Tanga, Gloria Gasper alisema tayari ofisi yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imetoa taarifa kwa wenyeviti wa Serikali za Vijiji vilivyo kando ya Bahari ya Hindi kuwataka wasiende baharini kufanya shughuli zozote ikiwamo uvuvi.
Alivitaja baadhi ya vijiji maarufu ambavyo wakazi wake wengi wanafanya shughuli nyingi baharini kuwa ni Kipumbwi, Fukwe za Wilaya ya
Pangani, Kigombe, Mkwaja na Pangani Mjini.
Maeneo mengine ambayo Sumatra imepeleka taarifa za tahadhari hiyo ni vijiji vya Wilaya ya Mkinga na katika Jiji la Tanga maeneo ya Sahare, Deap Sea,Chumvini, Chonoleani na Kasera.
“Tayari tumetuma taarifa za tahadhari hizo kwenye vijiji hivyo lakini pia tumewasiliana na vyombo vya habari kwa ajili ya kuwatangazia
wananchi wasithubutu kwenda baharini kabisa,” alisema Gloria.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constatine Massawe alisema shughuli zote zinazofanywa na wananchi baharini zimesitishwa hadi hapo watakapotangaziwa vinginevyo.
Kauli ya Serikali
Majira ya jioni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alilitaarifu Bunge kuhusu tishio hilo na kuwataka Watanzania wanaoishi karibu na fukwe za bahari kuchukua tahadhari.
“Taarifa hizi tumezipata kutoka idara yetu ya hali ya hewa na tutaendelea kupashana habari kadri muda unavyosonga. Watu wanaoishi mabondeni pia wanatakiwa kuchukua tahadhari kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha,” alisema Lukuvi.
Baada ya Lukuvi kutoa kauli hiyo ya Serikali, Mwenyekiti wa Bunge, Jenesta Mhagama alisema: “Tunaomba tuendelee kupashana habari kadri muda unavyosonga lakini tunahitaji kumwomba Mungu ili janga hilo lisitukute.”
Zanzibar giza
Wakati hayo yakiendelea Tanzania Bara, huko Zanzibar, umeme ulikatika nchi nzima na taarifa za awali zilieleza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa makusudi kupisha tishio hilo.
Hata hivyo, hakukuwa na kiongozi yeyote wa Serikali au Shirika la Umeme aliyekuwa tayari kuzungumzia hatua hiyo.
Kenya nayo yachukua hatua
Serikali ya Kenya jana pia ilitoa onyo kwa wananchi wake ikiwataka wasiende ufukweni kutokana na kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa fukwe kukumbwa na tsunami.
Wakazi wa Mombasa, Malindi, Lamu, Kiunga, Kilifi na Shimoni walitakiwa kuepuka mwambao wa Bahari ya Hindi kutokana na kukadiriwa kwamba viwango vya maji ya vinaweza kupanda hadi mita tatu.
Taarifa ya Serikali ilisema kutokana na makadirio ya mawimbi, kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa Pwani ya Kenya kukumbwa na tsunami.
“Kiwango cha maji kilitarajiwa kupanda hadi mita mbili na tatu katika maeneo ya Malindi, Lamu hadi Kiunga,” ilisema taarifa hiyo ya Serikali na kuongeza:
“Wavuvi wote na watu wakiwemo wafanyakazi wa hoteli, kampuni za watalii, michezo ya maji na maduka wanashauriwa kuondoka katika fukwe mara moja.”
Tayari nchi za Pwani katika Bahari ya Hindi zimeshauriwa kuchukua tahadhari baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 8.6 katika kipimo cha ritcher, kutokea chini ya bahari katika ufukwe wa Jimbo la Aceh, kaskazini mwa Indonesia.
Katika Pwani ya Bahari ya Hindi, nchi zilizokuwa katika orodha ya kukumbwa na tsunami ni Afrika Kusini, Tanzania, Kenya, Somalia, Kenya, Msumbiji.
Kituo cha Tahadhari cha Tsunami katika Pacific (PTWC), kilisema athari za janga hilo bado hazijajulikana.
Indonesia imewahi kukumbwa na tsunami mnamo mwaka 2004 na kusababisha vifo vya watu 170,000 katika kisiwa hicho cha Aceh.
Ofisa mmoja alinukuliwa na Shirika la Habari la Reuters, akisema sentimeta 17 (inchi 6.7) za tsunami zimetokea na mitetemo yake ilikuwa inaelekea katika Pwani ya Aceh.
Kituo cha Utafiti cha Marekani (USGS), kinachoweka kumbukumbu za matetemeko ya ardhi duniani kote, kilisema tetemeko la Aceh lilikuwa kwenye mzunguko wa kilometa 33 (maili 20) chini ya bahari, karibu kilometa 495 kutoka Banda Aceh, Makao Makuu ya jimbo hilo la Indonesia.
Imeandaliwa na Dismas Lyassa, Pamela Chilongola, Aidan Mhando na Patrica Kimelemeta, Geofrey Nyang’oro Dar na Burhani Yakub,Tanga