ULIMWENGUNI LEO: KUHUSU SYRIA


Silaha zanyamaza nchini Syria
Syria imesimamisha harakati za kijeshi ili kuutekeleza mpango wa kukomesha mapigano uliopendekezwa na mjumbe wa kimataifa anaesuluhisha katika mgogoro wa nchi hiyo, Kofi Annan.

 Ofisi ya Annan imethibitisha kuwa ilipokea barua kutoka kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad inaliyosema kwamba harakati zote za kijeshi  zitasimamishwa saa 12 leo asubuhi saa za Syria. 
Lakini utawala wa Assad umesema majeshi yake yatalipiza kisasi ikiwa yatashambuliwa na wapiganaji wa wapinzani. 

Kwa mujibu wa picha za mtandao, na taarifa kutoka ndani ya Syria mapigano bado yalikuwa yanandelea hadi hapo jana katika miji ya Homs,Hama na Rastan.    


Mawaziri wa G8 wajadili mgogoro wa Syria

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi  za G8 wanakutana kwa siku mbili mjini Washington ambapo wanalipa kipaumbele suala la Syria. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ameitaka Urusi ijitenge na utawala wa Rais Assad ambao amesema ni wa mauaji. 

Waziri Westerwelle pia ametoa mwito kwa nchi za G8 wa kutoa ishara ya kusimama pamoja dhidi ya Rais Assad. 

Umoja wa Mataifa umesema utawala wa Assad umeshawaua watu zaidi ya 9000 tokea mwezi  wa  machi mwaka jana. 

SUDAN

Wasiwasi juu ya kuendelea mvutano baina ya Sudan mbili

Umoja wa Afrika na Marekani zimetoa mwito kwa  Sudan na Sudan ya Kusini wa kukomesha mapigano kwenye mpaka wao.

 Sudan imetishia kuliandaa jeshi lake baada ya kutokea mapigano mengine kwenye mji wa mpakani wa Heglig. Majeshi ya Sudan ya Kusini yanadai kwamba yanalidhibiti eneo la mpakani lenye utajiri wa mafuta linalopiganiwa na nchi hizo mbili za Sudan. 

Eneo hilo linatoa hadi nusu ya mafuta ya Sudan yanayozalishwa kila siku. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon   amezitaka nchi mbili za Sudan ziwe na subira na  ametoa mwito wa kufanyika mkutano baina ya marais  wa Sudan Omar al- Bashir na wa Sudan ya Kusini  Salva Kirr. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia linajadidli jukumu lake la kulinda amani katika jimbo jirani la  Abyei.