Ndege ya ATCL yaanguka

Ndege pekee ya Shirika la Ndege la Tanzania "Air Tanzania" imepata ajali wakati ilipokuwa inajiandaa kuanza safari ya kutoka Kigoma kuelekea Dar es Salaam, kupitia Tabora.
Ajali hiyo ilitokea jana Jumatatu milango ya saa 4 na robo asubuhi kwa saa za eneo hilo, ikiwa na abiria 35 na wafanyakazi wanne.

Ndege hiyo iliteleza wakati ilipokuwa inajitayarisha kuruka. Wanawake wawili wazee wamekimbizwa hospitalini kutokana na mshituko waliopata.

Kuna taarifa mbalimbali zimetolewa kuhusu sababu ya ajali hiyo huku baadhi wakisema kuwa barabara ya kurukia ndege ilikuwa inateleza sana huku wengine wakisema kuwa kufeli kwa injini ya ndege ndiko kulikosababisha ndege hiyo ilale upande wa kulia na kuharibika sehemu ya mbele, bawa na injini ya pangaboi.


  • Abiria 41 wanusurika kifo
  • Yadaiwa chanzo ni tope, utelezi
WATU 41 waliokuwa ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), wamesurika kufa baada ya ndege hiyo kuanguka na kukatika vipande vipande kwenye uwanja wa ndege wa Kigoma jana.

Ndege yenye namba za usajili 5H – MWG, ilianguka mara baada ya kushindwa kuruka kutokana na kile kichodaiwa uwanja kujaa tope zito, lililosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.


Ndege hiyo, ilikuwa ikiruka kutoka Uwanja wa Kigoma kuelekea mkoani Tabora na hatimaye kurudi Dar es Salaam, ikiwa na abiria 35 na wafanyakazi sita, akiwemo rubani wa ndege hiyo, Kapteni Emanuel Mshana na msaidizi wake, Mbwali Masesa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Kihenya Kihenya, alisema uchunguzi wa awali unaonyesha huenda tope na utelezi ndicho chanzo cha ajali hiyo.

Alisema mwisho wa njia ya ndege kurukia, kulikuwa na tope zito, hali ambayo ilichangia kuifanya ndege hiyo ishindwe kuruka na hatimaye kuserereka na kutoka nje ya njia yake ya kurukia na kujikuta ikianguka vibaya.

“Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kulikuwa na tope zito ambalo inawezekana likawa chanzo cha ndege ile kushindwa kuruka na kujikuta ikiserereka hadi nje ya uwanja na kuvunjika vunjika,” alisema Kamanda Kihenya.

Kamanda Kihenya, alisema hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha na kwamba wote wako salama zaidi ya kupata mshutuko mdogo.

Alisema baada ya ajali hiyo, timu ya madaktari kutoka Hospitali ya Mkoa Maweni, walifika kwa ajili ya kuwafanyia vipimo.

Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Mkoa Kigoma, Elipid Tesha, alisema baada ya ndege kuanguka, magari ya Kikosi cha Zimamoto yaliwahi eneo la tukio na kuanza kumwaga maji ili kuepusha ndege hiyo kulipuka.

“Tulikuwa mbali kidogo, lakini nikiwa katika kituo cha Kampuni ya Synohadro, inayokarabati uwanja huo, niliona ndege imesimama katikati ya uwanja na ghafla niliona inaondoka kwa kasi.

“Nilishtuka mno kuona ule mwendo, kilichonishangaza ni pale nilipoona ndege inakaribia kumaliza uwanja bila kuruka, nilipata mashaka sana, ghafla niliona ikibiringika kwenye matuta nje ya njia ya kurukia,” alisema Tesha.

Kutokana na hali hiyo, alisema utaratibu unafanywa wa kuhakikisha, abiria waliokuwa wasafiri na ndege hiyo, wanaendelea na safari zao kwa kuwatafutia ndege nyingine.

Itakumbukwa Machi mosi, 2010, watu 46 walinusurika kifo baada ya ndege ya ATCL, waliyokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, kupata ajali wakati ikitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Ndege hiyo aina ya Boeing 737-200 yenye namba SH-Mvz, ilipata ajali hiyo saa 1:45 asubuhi, wakati ikitua tairi zake mbili zilipasuka na kusababisha kuacha njia yake, huku injini moja ya kushoto ikiingia maji.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia ajali hiyo, wakati ndege hiyo ilipokuwa ikitua kulikuwa na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha, ghafla kilisikika kishindo kikubwa kilichowashtua.

Kati ya watu hao walionusurika, 39 walikuwa ni abiria na saba wafanyakazi.