HALI ya Mbunge Clara Mwatuka aliyeugua ghafla na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, inaendelea vizuri licha ya kuwa bado amelazwa hospitalini hapo. Juzi, mbunge huyo aliugua ghafla akiwa katika semina ya wabunge kuhusu anuani mpya ya makazi, simbo za posta pamoja na teknolojia mpya ya utangazaji. Lakini jana, Mwatuka alilimbia gazeti hili kuwa anaendelea vizuri ingawa bado amelazwa katika hospitali hiyo akiendelea na matibabu. “Asante, naendelea vizuri lakini, bado nimelazwa hospitalini hapa, madaktari wakiendelea kunihudumia. Kwa kweli nawasifu madaktari wa Dodoma, wananipa huduma nzuri, bila shaka Mungu atanijalia kupona, naomba endeleeni kuniombea tu,’’alisema Mwatuka. Alisema kuwa mbali na shinikizo la damu vipimo vya madaktari vilionyesha kwamba alikuwa na Maralia, pamoja na vidonda vya tumbo, tatizo ambalo alisema linalomsumbua kwa muda mrefu. Hata hivyo, ingawa Mwituka hakutaka kueleza wodi alikolazwa, mwandishi wa habari hizi alifika hospitalini hapo na kubaini mbunge huyo alikuwa amelazwa wodi ya daraja la kwanza, ambayo hulazwa watu maarufu pamoja na wale wanaolipa ikiwa na utulivu, huku watu wakizuiwa kuingia ndani ya jengo hilo. Wakati huo huo, Bunge leo linaendelea na vikao vyake mjini Dodoma baada ya mapumziko ya mwisho wa wiki, ambapo Muswada wa Sheria ya Marekebisho wa Sheria Mbalimbali wa mwaka 2011 utawasilishwa. Kazi hiyo ilifanywa baada ya kumaliza kupitisha Muswada wa Marekebisho ya Utafiti wa Mifugo. Shughuli za leo za bunge zitatangulia kazi ngumu ya kesho ambapo, wabunge watachagua wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, ambao mchakato wake umekuwa mkali ndani ya Viwanja vya Bunge mjini hapa kwa wiki nzima. Katika mchakato huo, wagombea 33 wamepitishwa na Bunge kugombea Viti vya Ubunge wa Afrika Mashariki huku idadi inayotakiwa ni wabunge tisa. |
Post a Comment
Subscribe to:
Post Comments (Atom)