Serikali Yashtuka..Yagoma Kupokea Misaada yenye Masharti haya

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema Taifa halipo tayari hata kidogo kupokea misaada yenye masharti ambayo haiendani na mila na desturi za Kitanzania.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Ireland Mary Robinson pamoja na Mwanzilishi wa Taasisi ya Graca Machel, Craca Machel pamoja na ujumbe walioambatana nao Ikulu- Jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kuna baadhi ya wafadhili wanaisaidia Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na bajeti vizuri sana na bila masharti mabaya lakini kuna baadhi ya wafadhili wanaonyesha wazi kuwa wanataka Serikali ikubali masharti yao ambayo yanaenda kinyume na maadili ya taifa kitu ambacho hakiwezekani.
Amesema kutokana na changamoto hiyo Serikali itaendelea kusimamia maadili ya Taifa ipasavyo na imeweka mipango na mikakati mizuri kwa ajili ya kuongeza mapato yake ya ndani ili kuondokana na utegemezi kutoka kwa baadhi ya wafadhili ambao baadhi yao wanaahidi kuchangia bajeti kuu ya Serikali lakini mwisho hawafanyi hivyo.
Kuhusu Sekta ya afya, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali imeongeza maradufu bajeti yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 katika sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa viwango vinavyotakiwa nchini.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Ireland Mary Robinson pamoja na Mwanzilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya Graca Machel, Craca Machel waipongeza Serikali kwa jitihada inazozifanya katika uimarishaji wa sekta ya afya nchini na wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha huduma za afya nchini zinaendelea kuboreshwa ipasavyo.

from Blogger http://ift.tt/2v3h1Ox
via IFTTT