Shirika la uokoaji nchini Indonesia limesema hivi sasa miili 37 imepatikana kutoka kwenye bahari ya Java ambapo ndege ya Air Asia iliangukia mwishoni mwa juma lililopita.
Helikopta na Meli za kijeshi zimekuwa zikifanya doria katika eneo la bahari hiyo ambapo vitu vinavyoelezwa kuwa mabaki ya ndege vimeonekana.hali ya hewa ya eneo hilo kwa sasa imetengemaa ingawa bado mikondo ya bahari ina nguvu.
Vikosi vya wapiga mbizi wa Indonesia na Urusi vina matumaini ya kupata vifaa vya kurekodia mawasiliano ndani ya ndege, ambavyo vitasaidia kujua sababu ya kuanguka kwa ndege hiyo iliyokuwa ikisafiri kutoka Surabaya kwenda Singapore.
Air Asia ilikuwa imebeba Watu 162 ilipopata ajali.