Katika harakati za kuwasaida watu waliofikwa na maafa ya kimbunga cha
Haiyan katika kisiwa cha Ufilipino, Ujerumani imepeleka ndege kubwa
ikiwa na shehena ya tani 25 za mahitaji muhimu.
Waliokumbwa na maafa ya kimbunga Haiyan kisiwani Ufilipino
Watu zaidi ya alfu 10 wamekufa kutokana na kimbunga Haiyan katika kisiwa
cha Ufilipino. Jimbo la Leyte lililopo kati kati ya Ufilipino ndilo
hasa lilliloathirika na maafa yaliyosababishwa na dhoruba hiyo. Maalfu
kwa maalfu ya watu wanasubiri misaada huku wakiwa katika hali ya
kutamauka.
Ndege ya Ujerumani yatua Manila
Licha ya hali ngumu, watoaji misaada kutoka Ujerumani wameshaanza kutoa
huduma. Ndege kubwa ya Ujerumani ikiwa na shehena ya tani 25 za misaada
imeshatua katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila. Ndege hiyo imepeleka
mablanketi,mahema, dawa na vifaa kwa ajili ya tiba ya watu waliovunjika
mifupa.
Msaada huo umetolewa na mashirika mawili ya misaada ya Ujerumani .Pamoja
na shehena ya msaada , Ujerumani pia imewapeleka wataalamu
watakaoshughulikia na njia za kuwapatia watu maji safi ya kunywa.
Msemaji wa shirika husika la Ujerumani THW Bwana Nicolas Hefner ameeleza
kuwa watoaji misaada wa Ujerumani wamegawanyika katika makundi madogo
madogo yanayofanya tathmini ya hali katika sehemu mbalimbali
zilizokumbwa na maafa.
Matatizo yawakabili watoaji misaaada
Wahanga wa Kimbuga wajitahidi kuokowa vilivyobaki
Hata hivyo wanaotoa misaada wanakabiliwa na matatizo kama alivyoeleza
Maria Rüther wa shirika la misaada la Ujerumani linaloitwa "Aktion
Deutchland Hilft"
Amesema kwa sasa jambo muhimu ni usafirishaji wa mahitaji ya lazima,
lakini unakabiliwa na matatizo. Amesema hali hiyo inachelewesha shughuli
za usaidizi, na kwa hivyo inabidi kwanza kuviondoa vifusi barabarani
ili misaada iweze kufikishwa kwa watu. Kwa sasa misaada inawafikia watu
kwa taabu.Njia za mawasiliano zimeharibiwa kwa kiasia fulani.
Kiongozi wa shirika la misaada linaloitwa "Misereor," tawi la Asia
Ulrich Füßer amesema kwa sasa mambo yanasonga mbele polepole ,kwa sababu
ni vigumu kuitathmini hali yote jumla .Mashirika ya misaada ya
Ujerumani yanashirikiana na mashirika mengine kutoka duniani kote.
Katika kazi zao watoaji misaada kutoka mashirika ya Ujerumani
wanawasiliana na ubalozi wa Ujerumani mjini Manila.
Kwa sasa hakuna anaeweza kutoa tathmini ya uhakika juu ya kiwango cha
madhara na kiwango cha misaada inayohitajika.Hata hivyo Maria Rüther wa
shirika la "Aktion Deutschland Hilft" amesema mamilioni ya fedha
yatahitajika.
Marekani pia yasaidia
Wakati huo huo Marekani imepeleka Ufilipino manowari ya kubebea ndege ,
USS George Washington na manowari nyingine tano ili kushiriki katika
harakati za kuwasaidia watu waliokumbwa na maafa ya kimbunga cha
Haiyan.Wizara ya ulinzi ya Marekani imetoaa taarifa hiyo. Hapo awali
Marekani ilishatuma wanajeshi na ndege maalumu.