MTUHUMIWA ALIYEANDIKA NA KUSAMBAZA TAARIFA ZA UVUMI KWENYE MITANDAO YA KIJAMII JUU YA KULISHWA SUMU KWA MKUU WA MAJESHI YA ULINZI NA USALAMA GEN. DAVIS MWAMUNYANGE AKAMATWA.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia kwa mahojiano mtuhumiwa aliyetengeneza/andika maneno ya uvumi na uzushi na kisha kuyasambaza katika mitandao ya kijamii kama FACEBOOK, WHATSAPP, n.k kwamba Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Generali DAVIS MWAMUNYANGE amenusurika kifo baada ya kulishwa sumu.
Baada ya taarifa hizo kupokelewa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kupitia dawati la makosa ya mitandao Makao Makuu ya Polisi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) walianza kufuatilia mawasiliano ya kimtandao hadi ilipobainika nini chanzo cha taarifa hiyo. Baada hapo msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa ulianza hadi tarehe 02/10/2015 alipokamatwa huko Arusha. Mtuhumiwa huyu jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.
Taarifa za awali zinaonyesha kuwa mtuhumiwa huyo ni mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza katika moja ya Taasisis za elimu ya juu nchini. PiaBaada ya kukamatwa alipekuliwa na kukutwa akiwa na Kompyuta Mpakato (LAPTOP) aina ya HP na simu ya mkononi.
Aidha,katika mahojiano ya hayo mtuhumiwa amekiri kuusambaza ujumbe huo. Upelelezi juu ya shauri hili unaendelea na utakapokamilika jalada la kesi hii litafikishwa kwa mwanasheria wa serikali ili sheria ichukue mkondo wake.
S. H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM