Timu ya soka ya Burkina FC imeendelea kufanya vibaya katika michezo yake mitatu ya ligi daraja la kwanza Tanzania bara msimu wa mwaka 2015/2015 baada ya kuruhusu kufungwa michezo miwili na kulazishwa sare moja katika uwanja wake wa nyumbani wa jamhuri Morogoro.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili mjini hapa, Kocha wa klabu hiyo, Alan Yahaya alisema sio jambo geni katika ligi timu kupoteza michezo mitatu ama zaidi ya hapo kwani hilo ndilo soka lilivyo.
Yahaya alisema kuwa wamepoteza michezo miwili kwa kufungwa na Polisi Moro SC katika mchezo wa ufunguzi kisha kulazimishwa sare na Kimondo FC ya Mbeya kabla ya kupoteza mchezo mwingine dhidi ya Njombe Mji na wana uhakika wa kufanya vizuri katika michezo ijayo.
“Soka imekuwa ikitoa matokeo ya kustajabisha katika viwanja vingi duniani na kwa upande wa Burkina limejitokeza katika michezo mitatu ya ligi daraja la kwanza lakini Burkina itafanya vizuri katika michezo inayofuata ya ligi hiyo.”alisema Yahaya.
Yahaya alisema kuwa timu ya Burkina imekuwa ikianza vibaya katika ligi hiyo hasa michezo ya mwanzo na kuwataka mashabiki, wapenzi na wadau kutokata tamaa na timu yao kwani michezo bado ipo mingi na makosa yanayojitokeza katika michezo hiyo, benchi la ufundi linaendelea kuyafanyia kazi ili michezo ijayo iweze kupata ushindi.
Akizungumzia juu ya ushiriki wa timu yao katika ligi hiyo, Yahaya alisema kuwa Burkina FC kwa sasa inahitaji msaada wa hali na mali wa kuisaidia timu hiyo ili iweze kushiriki vyema michezo ya ligi hiyo.
“Hii timu ni kama imesuswa na viongozi wa soka kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya na imekuwa ikipata adha mbalimbali za kuendesha timu hiyo katika michezo yake ya ligi daraja la kwanza tangu iingie katika ligi hiyo miaka tisa iliyopita.”alisema Yahaya.