10412002_789494981096465_7678104604296404163_n
Jakaya-Kikwete1
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Septemba 10, 2015 amepokea tuzo nyingine ya kimataifa, siku mbili tu baada ya kupokea tuzo ya kutambua mchango wake katika kudumisha amani na utulivu katika Tanzania.
Rais amekabidhiwa tuzo hiyo ya Uongozi na Utawala Bora na Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa AshaRose Migiro ambaye aliipokea kwa niaba ya Rais Kikwete katika sherehe iliyofanyika Julai 25, mwaka huu, 2015, Afrika Kusini.
Rais Kikwete ametunukiwa tuzo hiyo na Bodi ya Uongozi ya African Achiever’s Award kwa kutambua mchango wake katika maeneo ya uongozi na utawala bora wakati wa uongozi wake wa miaka 10 wa Tanzania.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika Ikulu, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, miongoni mwa viongozi waliohudhuria, ni Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Yohana Sefue, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ndugu George Masaju, Kaimu Katibu Mkuu Ikulu Ndugu Susan Mlawi na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Ndugu Tom Bahame Nyanduga.
Akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hiyo,Waziri Migiro amesema kuwa kwa kupata tunuku hiyo sasa Rais Kikwete anajiunga na waafrika wengine mashuhuri ambao wamepata tuzo hiyo ambao ni Rais wa zamani wa Ghana, Hayati John Atta Mills, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Mama Nkozana Dlamini Zuma na aliyekuwa kiongozi wa Kanisa la Anglikana na Duniani na mwanaharakati mashuhuri waAfrika, Askofu Mkuu Desmond Tutu.
Waziri Migiro amesema kuwa Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa Waafrika mashuhuri 1,202 ambao majina yao yalipendekezwa kwa ajili ya kutunukiwa tuzo hiyo kwa mwaka huu lakini Bodi iliyomtunukia Rais Kikwete tuzo hiyo imeridhishwa zaidi na mchango wake mkubwa katika kujenga na kuleta utawala bora katika miaka yake 10 ya uongozi wa Tanzania.
Amesema kuwa miongoni mwa vigezo vikuu vya tunuku hiyo ni jinsi Rais Kikwete alivyosimamia utawala wa sheria, alivyochangia kujenga demokrasia nchini, uongozi wake ulivyopambana na rushwa, ulivyoheshimu haki za binadamu, ulivyokuwa stahimilivu na ulivyoinua uhuru wa kila aina nchini.
Waziri Migiro pia amezungumzia maudhui ya mada ambayo Rais Kikwete aliitoa baada ya kutunukiwa tuzo hiyo ambayo kichwa chake cha habari kilikuwa African Unity: Prospects and Challenges (Umoja wa Afrika: Fursa na Changamoto) ambako miongoni mwa mambo mengine Rais alithibitisha uhusiano kati ya ustawi ama umasikini na utulivu katika Bara la Afrika.
Rais pia alizungumzia kuhusu hamu yake ya kustaafu baada ya kumaliza ngwe ya uongozi wake, akisisitiza kuwa hiyo ni sehemu ya utamaduni na ustawi wa demokrasia ya Tanzania na kuwa kwa sababu ya uvumilivu wa uongozi hakuna Rais yoyote wa Tanzania amepata kulazimika kukimbia nchi kwenda kuishi uhamishoni.
Naye Rais Kikwete amesema kuwa hakuweza kwenda mwenyewe kupokea tuzo hiyo kwa sababu wakati huo alikuwa katika ziara rasmi ya Kiserikali katika Australia lakini akaongeza kuwa amefurahi kutunukiwa tuzo hiyo.
Amesema kuwa tunuku hiyo ni ya Watanzania na yeye ameipokea tu kwa niaba yao na kwa niaba ya Serikali yake ambayo ndiyo imechangia kuboresha utawala bora chini ya uongozi wake.
“Mimi naipokea tuzo hii kwa niaba ya Watanzania. Wao ndio washindi wa kwelikweli wakiongozwa na Serikali yao ambayo imefanikisha kudumisha utawala bora katika miaka 10 iliyopita.Wenzetu wametupima kwa kutulinganisha na wengine na tukaonekana bora. Nawashukuru sana kwa imani yao kwetu.”
Tuzo hiyo ya Uongozi na Utawala Bora imekuja siku mbili baada ya Rais kupokea Nishani ya Amani na Utulivu iliyotolewa kwake na Taasisi ya East Africa Book Records yenye makao makuu yake Uganda na kukabidhiwa kwa Rais Kikwete na mtendaji wake mkuu, Dkt. Paul Bamutize.
Akitunuku nishani hiyo juzi, Jumanne, Septemba 8, 2015 katika hafla nyingine iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Dkt. Bamutize alisema kuwa amani na utulivu ambao Rais Kikwete na Serikali wamejenga katika Tanzania imeleta matumaini kwa wawekezaji na majirani wa Tanzania na kuwa mfano dhahiri wa kuigwa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na mabalozi wa Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
10 Septemba, 2015