Na Maelezo
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema serikali inahamasisha wanawake kujiendeleza kinadharia na kivitendo ili kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa kisasa unaohitaji wafanyakazi wenye ujuzi wa maarifa ya sayansi na teknolojia kwa lengo la kijikwamua kiuchumi.
Akizungumza huko Kibokwa Kinyasini Wilaya ya Kaskazini A Unguja katika sherehe za uwekaji wa Jiwe la Msingi wa Kituo cha Kufundishia Wanawake Utengenezaji wa Vifaa vya Umeme wa Jua Amesema serikali imeanzisha kituo hicho ili wanawake waweze kupiga hatua kubwa zaidi na kuonyesha uwezo wao ndani na nje ya nchi.
Amesema lengo la kituo hicho ni kuendeleza rasilimali watu kwa kuwajengea uwezo na kuwawezesha wanawake wa vijijini kutengeneza vifaa vinavyotumia umeme wa jua vikiwemo taa, mashine na majiko ya kupikia kwa lengo la kujikwamua kimaisha.
Mhe Balozi amesema kituo hicho kinatarajia kuwajengea uwezo wa kitaalamu wanawake 16 kutoka katika vijiji 8 vitakavyochaguliwa kwa kila nusu mwaka na baadae kueneza ujuzi huo kwa wanakijiji wenzao watakaohitaji huduma hiyo.
“Mpango huu utawawezesha wanawake wa vijijini kuondokana na umasikini na kuwawezesha kiuchumi na hivyo kuyafikia malengo ya Dira ya 2020 na Mkuza”, amesema Balozi Seif.
Aidha Balozi Seif ameeleza kuwa ujuzi na elimu ndivyo vitakavyowawezesha wananchi kufikia uchumi wa kisasa na kutambua uwezo na nguvu kubwa ya wanawake katika mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Amefahamisha kuwa kituo hicho kitakua ni cha kwanza cha aina yake Afrika Mashariki Kusini na Kati ambacho kinatarajiwa kuwajengea uwezo wa kitaalamu wanawake wa vijiji mbalimbali.
Mradi huo wa kituo cha mafunzo ya wanawake ya kutengenezea vifaa vya umeme wa jua unatekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya India kupitia Chuo cha Barefoot cha India na Washirika wa Maendeleo UN Women ambao umegharimu shilingi milioni 400 za kitanzania.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI ZANZIBAR