Dk Shein : Sekta ya uvuvi kuimarishwa


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Pemba                                                                                                           5.1.2015
UJENZI  wa masoko mapya ya  kisasa ya samaki ni miongoni mwa mikakati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika azma yake ya kuimarisha sekta ya uvuvi na kuongeza tija sambamba na kuongeza soko la ajira kwa wananchi wake.
 
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kulizindua soko jipya la kisasa huko Tumbe, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 
 
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema  kuwa ujenzi wa soko hilo utawanufaisha zaidi wavuvi wa Tumbe pamoja na maeneo mengine pamoja na kupanua soko la ajira kwa wakaazi wa Tumbe na vitongoji vyake ambapo hatua hiyo ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
 
Dk. Shein alisema kuwa kabla ya mwaka 1963 Zanzibar ilikuwa haijatawaliwa na ilikuwa na viongozi wake wa asli na ndipo baadae ukaja utawalakutoka Ureno na kufuatia Sultani kutoka Oman na kusisitiza kuwa hivi sasa Zanzibar iko huru na hakuna mtu yoyote wa kuja kuitawala tena Zanzibar.