Mbunifu wa kimataifa wa mavazi kutoka Tanzania,
Sheria Ngowi amedhihirisha kuwa yeye ni nguli katika ubunifu baada ya
kufinika katika onyesho la mavazi la kimataifa lijulikanalo kama Mercedes
Benz Fashion Week Africa 2014 lililofanyika juzi Ijumaa mjini Johannesburg,
Afrika Kusini.
Ngowi alionyesha mkusanyiko wa mavazi aliyoyaita
'PRIDE' yaani kujivunia, kama moja ya njia za kumuenzi Baba wa Taifa, Mwl.
Julius Nyerere pamoja na viongozi mashuhuri waliopigania uhuru
Afrika.
Afrika Kusini ilizizima na kuduwaa kwa muda
usiopungua dakika 15 pale ambapo mavazi mbali mbali yaliyobuniwa na Ngowi
yalipokuwa yakioneshwa katika ukumbi wa Melrose
Arch.
Sheria Ngowi alionyesha mkusanyiko wa mavazi aina ya
suti yenye ubunifu na ueledi wa hali ya juu kwa kutumia vitambaa vya kisasa
na kale vilivyonakshiwa kwa maua na rangi za kuvutia kama nyekundu,
zambarau, machungwa, nyeupe na nyeusi huku mengine yakiwa bila maua lakini
yaliyong'aa kwa kutumia rangi imara kama blu, kahawia na
kijivu.
Onyesho hilo la Mercedes Benz Fashion Week Africa
2014 lilihudhuriwa na watu mbali mbali wakiwemo viongozi wa umma kutoka
Afrika kusini, Balozi wa Tanzania Afrika Kusini, Radhia Msuya, wabunifu wa
mavazi kutoka nchi za Afrika kama Taibo Bacar kutoka Mozambique, David
Tlale kutoka Afrika Kusini, waandishi wa habari kutoka sehemu mbali mbali
za dunia na wadau wa mitindo.
Mercedes Benz Fashion Week Africa 2014 ni onyesho la
kimataifa linalofanyika nchini Afrika Kusini mara moja kwa mwaka
likikusanya zaidi ya wabunifu wa mavazi 35 kutoka Afrika kwa ajili ya
kuonesha ubunifu wa mavazi yao ambapo kwa mwaka huu Sheria Ngowi ni mbunifu
pekee aliyechaguliwa katika onyesho hilo kutoka
Tanzania.
Sheria Ngowi anasifika kwa ubunifu wa mavazi aina ya
suti, kanzu,sare za makampuni, mashirika, shule na hafla mbalimbali kama
harusi.Mbunifu huyu alifungua rasmi ofisi zake zilizopo Masaki, mtaa wa
Buzwagi mkabala na Ubalozi wa Angola mwaka mmoja na nusu uliopita ambapo
alianza kazi kwa kuwatengenezea mavazi watu kutoka nchi mbalimbali
duniani.
Pongezi nyingi kwa Sheria Ngowi, unaipeperusha vyema
bendera ya Tanzania kwa kipaji chako na kazi zako
nzuri.