China na hatua dhidi ya Ebola

China itawaweka karantini kwa siku 21, watumishi wake wa huduma ya afya  wanaowashughulikia wagonjwa wa Ebola katika Afrika magharibi, baada ya kurejea  nyumbani. Naibu mkurugenzi katika wizara ya  afya anayehusika na  udhibiti na kinga ya maradhi ya kuambukiza he Qinghua ,  aliwaambia waandishi habari kwamba   kwa kuwa madaktari wanahusika na  upimaji wa virusi vya  Ebola, watalazimika kuwekwa karantini kwa siku 21 ili wachunguzwe  na yeyote atakayegunduliwa kuwa na dalili za Ebola atapelekwa moja kwa moja kwenye hospitali maalum. China  imetuma Afrika magharibi wafanyakazi 30 wa afya na inapanga kupeleka mamia wengine mnamo wiki zijazo. Kwa upande mwengine wanajeshi wa Kimarekani wanaofanya kazi Afrika magharibi pia watawekwa karantini watakaporejea nyumbani, wakati Australia imezuwia kuingia nchini humo kwa raia kutoka nchi tatu zilizoathirika zaidi na Ebola huko Afrika magharibi. Nchi hizo ni Sierra Leone, Liberia na Guinea. Kwa mujibu wa Shirika la afya duniani-WHO, karibu watu 5,000 wamefariki dunia kutokana na janga hilo la karibuni la maradhi ya  Ebola.