MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani
Njombe, Anthony Mahwata ameiambia mahakama ya Hakimu Mkazi ya wilaya ya Njombe
kwamba kesi aliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa zamani wa Jimbo la Njombe
Magharibi, Yono Stanley Kivela imelenga kumchafua kisiasa.
“Mheshimiwa hakimu, mashahidi mbona wanatengeneza ushahidi
unaotofautiana ili kuniharibu kisiasa, Yono anatengeneza ushahidi wa uongo ili
kuniharibia kisiasa, mashahidi wote ni wakutengenezwa hawana kumbukumbu,” alisema
Mahwata wakati alipopanda kizimbani kujitetea katika kesi inayomkabili ya
kutishia kuua.
Mahwata aliiambia mahakama hiyo kwamba; “Mimi ni kweli
nilimpinga Yono ubunge kwa sababu hana uwezo katika jimbo letu. Jambo jingine
linalonisikitisha mheshimiwa ni la Yono kuwaleta waandishi wa habari, amediriki
kunichafua kwamba mimi nimefungwa kwa kurusha katika sms (meseji) katika
mitandao ya kijamii ili mimi nisiweze kusikika kisiasa, mimi sikumfukuza
Igwachanya Sekondari, yote aliyosema ni ya uongo.”
Akitoa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo,
Augustino Rwizile alisema Februari 5, mwaka 2013 alipigiwa simu na Mkuu wa
wilaya ya Wanging’ombe, Esterina Kilasi akimuuliza kama anayo taarifa ya ujio
wa timu ya mpira wa miguu ya Yanga Veteran kuja kucheza katika shule ya
sekondari Igwachanya na hivyo aende kufatilia na alimwambia mkuu huyo wa wilaya
kwamba hana taarifa za ujio wa timu hiyo.
Kevela anawashtaki Mwenyekiti Mahwata na mwenzake Evarist
Makurumbi ambaye mwaka jana alikuwa ni Mwenyekiti wa timu ya mpira wa miguu ya
kijiji cha Igwachanya kwa kutishia kumuua na pia kusababisha uvunjifu wa amani
kabla ya mchezo wa soka uliozikutanisha Yanga Veteran ya Jijini Dar es Salaam
dhidi ya Igwachanya.
Awali akisoma mashtaka dhidi ya washtakiwa hao, Wakili wa
serikali, Atu Mwakasitu kuwa mnamo Februari 5, 2013, Mahwata na Makurumbi
wakiwa katika uwanja wa shule ya sekondari Igwachanya na baadaye kuhamia kwenye
uwanja wa mpiwa wa miguu wa kijiji cha Igwachanya walihatarisha uvunjifu wa
amani kwenye uwanja huo baada ya kuweka magari yao mawili aina ya RAV 4 namba
T749 AYU na NOAH namba T973BGG na kwenda kuyaweka katikati ya magoli ya mpira
kwenye uwanja huo kuzuia mchezo usichezwe.
Naye mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Makurumbi
aliiambaia mahakama hiyo kuwa mashahidi walioletwa na Kevela kwa ajili ya kutoa
ushahidi dhidi yake juu ya mashtaka yanayowakabili yeye na mwenzake wamekuwa
wakitofautiana na kwamba ushahidi uliotolewa umetengenezwa.
“Mheshimiwa shahidi wa kwanza Yono aliileza mahakama kwamba
alipofika uwanjani alikuta kuna gari mbili zimepaki, lakini Rikiz Majimwema
alisema alisema gari zile zipo mbele yake, lakini zilimpita na kwamba aliziona
zimepaki golini na kamuona aliyezipaki,” alisema Makurumbi.
Mshtakiwa huyo aliiambia pia mahakama hiyo kwamba, shahidi
mwingine ambaye hamkumbi alidai anazo picha alizopiga akionyesha magari hayo
mawili yamepaki kwenye magoli ya uwanja huo, lakini zilipokuja kuonyeshwa
mahakamani hapo alizikana kwa sababu zinaweza kuwa ziliunganishwa kwa sababu
technolojia inawezekana kufanya hivyo.
Hata hivyo washtakiwa hao ambao wako nje kwa dhamana
walitakiwa kuja na mashahidi wao, lakini mashahidi hao hawakutokea mahakamani.
Hakimu Rwizile ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 27, mwaka huu baada ya
washatakiwa hao kutakiwa kuja na mashahidi wao.