WATUMISHI WASIMAMIWE MAADILI YA KAZI

MKUU wa mkoa wa Njombe, Kapteni Mstaafu, Aseri Msangi amewataka waajiri wasimamie kazi vizuri na kuwa tayari kutoa motisha kwa watumishi wanaofanya kazi vizuri sambamba na kutoa adhabu kwa watumishi wanaokiuka taratibu za kazi.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao pili cha baraza la wafanyakazi ofisi ya mkuu wa mkoa wa Njombe kilichofanyika kwenye ukumbi wa Day to Day mjini hapa, Msangi pia amekemea baadhi ya watumishi wa umma wasizingatia maadili ya mavazi kwenye ofisi za umma hususan wafanyakazi wanawake.

"Nikuombe RAS 'Katibu Tawala mkoa" kanuni za maadili zifuatwe kwa watumishi wote,hatuji kufanya mapenzi ofisini, watu wengine hawatafanya kazi wanakuangalia wewe," alisema Msangi.

Mbali na kuhimiza maadili kazini, Mkuu huyo wa mkoa alitoa rai kwa wafanyakazi wa serikali hapa nchini kutumia vizuri mikopo wanayokopa kutoka katika Saccos ili kuendelea kukabiliana na matatizo pamoja na janga la umasikini.

Katika hatua nyingine, Msangi aliwaambia wajumbe wa Baraza hilo la Wafanyakazi kuwa mkoa wa Njombe umeongezewa siku za zoezi la utoaji wa chanjo ya Surua na Rubella mpaka Oktoba 26, mwaka huu.

Msangi alisema sababu za kuongezwa kwa siku hizo mbili zilitokana na upungufu wa dawa za chanjo ambazo walilazimika kuagiza kutoka bohari kuu ya dawa mkoani Iringa.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Jackson Saitabahu ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza hilo, ameagiza chama cha wafanyakazi kuwahimiza wafanyakazi kupima maambukizi ya VVU ili waweze kupatiwa huduma kirahisi.

Alisema kama mkoa wanajipanga zaidi kupata takwimu sahihi ya maambukizi ili kuona kama imeshuka ambapo awali ilikuwa ni asilimia 14.8 na mkoa kutajwa kuongoza kwa kasi maambukizi ya ukimwi.