Marekani yakaribisha makubaliano ya serikali ya kitaifa nchini Afghanistan
Marekani imeukaribisha mpango wa kugawana madaraka uliomtangaza waziri wa fedha wa zamani Ashraf Ghani kuwa rais mpya wa Afghanistan, na kutumai kwamba mkataba na Marekani kuhusu ulinzi, uliokumbwa na utata utatiwa saini wiki ijayo. Ghani na mpinzani wake Abdulla Abdulla walitia saini makubaliano hayo siku ya jumapili na kumaliza miezi mitatu ya uchaguzi ulio na utata ulioikwamisha nchi hiyo wakati ambapo wanajeshi wa kigeni wanaoongozwa na Marekani wakimaliza muda wao wa takriban miaka 13, wa mapambano dhidi ya wanamgambo wa Taliban. Serikali ya muungano nchini Afghanistan inatoa nafasi ya makubaliano ya pamoja ya usalama yatakayotoa nafasi ya kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan baada ya kumaliza muda wao mwishoni mwa mwaka huu, jambo ambalo rais anayeondoka Hamid Karzai alikataa kulitia saini. Kulingana na makubaliano hayo Abdulla Abdulla atachukua nafasi mpya ilioundwa ya mtendaji Mkuu ambayo ni sawa na ile ya Waziri Mkuu.