Jeshi la Israel limesema limeiangusha ndege ya kivita ya Syria
katika milima ya Golan, ikisema ilikuwa imevuka mpaka wa usitishaji
mapigano katika eneo linalokaliwa na Israel. Hili ni tukio kubwa zaidi
kutokea katika eneo hilo tangu kuanza vita vya wenyewe kwa
wenyewe nchini Syria mwaka wa 2011.
Taarifa iliotolewa na jeshi la
Israel ambayo haikuwa na maelezo zaidi ilisema ndege hiyo iliyoingia
eneo la Israel ilifanikiwa kudunguliwa muda mchache kwa mfumo wa
kujilinda wa angani karibu na mpaka wa Syria. Kudunguliwa kwa
ndege hiyo kunakuja wiki tatu baada ya Israel kuiangusha ndege
nyengine isokuwa na rubani iliokuwa katika anga ya milima ya Golan
wakati mapigano yakipamba moto upande wa Syria, ambapo eneo
kubwa linashikiliwa na waasi wanaopigana kuuangusha utawala wa
Bashar Al Assad. Syria imethibitisha kuangushwa kwa ndege yake
ya kivita na kukielezea kitendo hicho kuwa cha uchokozi.