Idadi ya wakimbizi wa Syria waongezeka Uturuki

Naibu waziri Mkuu wa Uturuki Numan Kurtulmus, amesema idadi ya wakimbizi wa Syria waliofika nchini humo siku nne zilizopita wakikimbia kuuweko kwa wanamgambo wa dola la kiislamu wamefikia 130,000. Naibu waziri mkuu huyo amesema Uturuki imejitayarisha kukabiliana na hali mbaya zaidi iwapo wakimbizi wa Syria wataongezeka. Wakimbizi wamekuwa wakiingia nchini humo kuanzia Alhamisi iliopita wakikimbia mashambulizi ya wanamgambo wa IS yanayoonekana kusogea mpakani mwa Uturuki. Wanamgambo hao waliojitenga kutoka kwa kundi la kigaidi la Al Qaeda na kuunda kundi lao la IS na kutangaza utawala wa sheria za kiislamu, linaloongoza kupitia sheria kali za kiislamu katika maeneo inayoyadhibiti mpakani mwa Syria na Iraq, katika siku za hivi karibuni limesogea mbele katika maeneo ya Syria yanayopakana na uturuki, ambapo wakimbizi wameripoti juu ya mauaji ,ikiwa ni pamoja na kupigwa mawe, kukatwa vichwa na kuchomwa makaazi ya watu.