SHULE YATAKA KUHAMISHWA KATIKA ARDHI YA WANANCHI

KANISA la Waadventista Wasabatho (SDA) linalomiliki Shule ya Sekondari Ndembela wilayani Rungwe limeamuliwa kuondoa shule hiyo kwenye majengo na ardhi inayomilikiwa na wananchi wa Kijiji cha Ndembela, kata ya Makandana wilayani Rungwe.

Uamuzi huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispine Meela wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ndembela kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu.

Kwa zaidi ya miaka 16 sasa kumekuwepo na mgogoro baina ya kanisa hilo na wananchi wa kijiji cha Ndembela kuhusiana na umiliki wa shule hiyo ambayo awali ilikuwa ya umma lakini mwaka 1994 ikakabidhiwa kwa kanisa hilo ili waiendeshe.

Akifafanua kuhusu sakata hilo,  Meela alisema kuwa baada ya Serikali kuikabidhi shule hiyo kwa uongozi wa Kanisa la SDA, pia kanisa liliruhusiwa kuifanyia usajili, hivyo shule hiyo ni mali halali ya kanisa hilo.

Hata hivyo  Meela, alisema kuwa ardhi na majengo ya shule hiyo bado ni mali halali ya Serikali ambayo kwa niaba yake inapaswa kusimamiwa na wananchi wa kijiji cha Ndembela.

“Shule ya Sekondari Ndembela kama taasisi ni mali halali ya Kanisa, lakini properties (mali) kama vile majengo na ardhi ni mali ya umma na hivyo tunalitaka kanisa liondoe shule yake kwenye majengo na ardhi ya umma,” alisema Meela.

Alisema awali wananchi walifanya makosa kudai shule hiyo na ndiyo sababu kesi ilipopelekwa mahakamani, mahakama iliamua kuwa shule ni mali ya kanisa, lakini kama suala lingekuwa ni mali, hakuna shaka kuwa wananchi wangepewa ushindi.

Awali akisoma risala ya wananchi hao, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Dornad Mwakasaka, alisema kuwa wananchi hawana haja na shule hiyo, isipokuwa wanataka warejeshewe ardhi na majengo yao  ili wayatumie kwa maslahi yao na vizazi vijavyo.

Alisema kuwa wananchi hao wametumia njia za amani kudai haki hiyo kwa miaka zaidi ya 16 na sasa wameanza kuishiwa na uvumilivu na kuwa wako tayari hata kumwaga damu ili kuhakikisha wanarejesha ardhi na majengo hayo mikononi mwao.

“Tumefuatilia haki yetu hii kwa muda mrefu lakini tunapuuzwa na Serikali, huku Kanisa hili likizidi kukalia ardhi na majengo yetu kwa nguvu, sasa tumeishiwa na uvumilivu na kama hatupati suluhu sasa tutatumia nguvu ya umma kurejesha mali yetu,” alisema Mwasaka.

Baada ya Hotuba ya Mkuu wa wilaya, wananchi hao walionyesha kufurahishwa na uamuzi huo, hivyo kuweka kando hasira na mipango yao ya kuvamia shule hiyo kwa lengo la kuwatimua kwa nguvu viongozi wa kanisa hilo.