MFUMO MPYA WA UTOAJI WA RUZUKU WAFURAHISHA WANARUNGWE




WANANCHI wilayani Rungwe wamefurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kufuta utaratibu wa kuwatumia mawakala kusambaza pembejeo za ruzuku kwa wakulima wilayani humo, kwa madai kuwa utaratibu huo haukuwa na tija kwa wananchi masikini.

Kauli ya wananchi hao imefuatia tangazo la Mkuu wa Wilaya hiyo Chrispine Meela kuwaeleza wananchi kuwa Serikali imeufuta mfumo huo na badala yake ruzuku itatolewa kupitia kwenye vikundi vya wananchi ambavyo vitapewa mikopo isiyokuwa na riba za kibiashara.
Mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispine Meela

Meela alitoa tangazo hilo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ndembela kilichopo kata ya Makandana wilayani humo alikokuwa akizungumza na wananchi.

Meela aliwataka wananchi hao kuanza kuunda vikundi vidogo vidogo ili fedha za ruzuku zitakapotolewa na Serikali waweze kukopeshwa na kuzitumia kununulia pembejeo za kilimo kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo.

Wakizungumza na Nipashe baada ya tangazo hilo la Mkuu wa Wilaya, wananchi hao walisema kuwa mfumo wa kusambaza mbegu na mbolea za ruzuku kwa kuwatumia mawakala uliwakandamiza watu masikini na wale wasiokuwa na uwezo wa kujieleza kwenye vikao vya kamati za mbolea za vijiji.

Dornald Mwasaka (61) alisema kuwa amefurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kufuta utaratibu wa kusambaza mbolea kwa kuwatumia mawakala kwa sababu mawakala walikuwa wakichakachua vocha za ruzuku hali ambayo ilisababisha mbolea isiwafikie walengwa.

“Baadhi ya mawakala badala ya kuleta mbolea walikuwa wakija kununua vocha kwa bei nafuu kutoka kwa wakulima na kuzipeleka benki, hali hiyo ilisababisha mbolea isifike vijijini, kwa kweli nimefurahishwa kuona utaratibu huo umefutwa,” alisema Mwasaka.

Mwananchi mwingine, Yusta Bulambo alisema kuwa utaratibu mpya uliotangazwa na Mkuu wa Wilaya anaona ni mzuri ingawa wananchi bado hawajahamasishwa vya kutosha kujiunga kwenye vikundi.

“Nikiangalia hapa kijijini kwetu hakuna vikundi hivyo vinavyosemwa, ingawa utaratibu mpya unaonekana ni mzuri, lakini wasiwasi wangu ni kwamba bado sisi wananchi hatujaanzisha vikundi vinavyotakiwa na hivyo tunaweza kunyimwa fedha za mikopo kwa kutotimiza mashariti ya kujiunga kwenye vikundi,” alisema Bulambo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Makandana, Boniphas Mwasikili alisema kuwa utaratibu mpya utawasaidia wananchi wake kupata mbolea kwa kuwa utaratibu wa zamani ulikuwa na dalili za ubaguzi.

“Katika utaratibu wa Vocha, kamati ya Mbolea ndiyo ilikuwa inachagua watu wa kupewa ruzuku, sasa hapo inawezekana kamati ikachagua kwa ubaguzi, lakini sasa kwa sababu mbolea itatolewa kwa mkopo, kila mwananchi mwenye uwezo ataipata,” alisema Diwani Mwasikili.