MIRADI YA MAENDELEO YASUASUA MBARALI





BAADHI ya miradi iliyoidhinishwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha, bado utekelezaji wake haujakamilika licha ya kuwa miradi hiyo haikuingizwa kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
MKURUGENZI WILAYA MBARALI ADAM MGOYI KATIKA

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Adam Mgoyi wakati wa kikao cha kawaida cha baraza la Madiwani kilichokutana jana mjini Rujewa kwa ajili ya kupitisha makadilio ya bajeti ya Halmashauri hiyo kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2013/2014
 
Alisema kuwa miradi hiyo bado haijafa na kuwa itaendelea kutekelezwa kama ilivyokusudiwa kwa madai  kuwa fungu lake lilishatengwa.
Mgoyi alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya baadhi ya madiwani kuanza kuilalamikia Serikali kuwa haitoi fedha za miradi ambayo imeombewa fedha na Halmashauri hiyo kwa wakati na kusababisha miradi hiyo kudolora.

Awali baadhi ya madiwani hao walitoalionyesha wasiwasi wao juu ya miradi ambayo ilikuwa bado haijakamilika, huku kwenye bajeti inayoandaliwa ikiwa haijaingizwa.

Kwenye malalamiko yao madiwani hao walisema kuwa kuna maeneo mengi ambayo miradi hayajatekelezeka kutokana na kukosa fedha za uendeshwaji katika bajeti ya mwaka wa fedha unaomalizika, hali inayotia shaka kama miradi mipya iliyoingizwa kwenye bajeti ya mwaka ujao itatekelezwa.
 
Baadhi ya miradi iliyotiwa shaka na madiwani hao ni pamoja na ujenzi wa shule za msingi, Nyumba za walimu na baadhi ya muindombinu ya barabara ambayo walidai kuwa bado haijatekelezeka.

Katika ufafanuzi wake Mgoyi alisisitiza kuwa miradi hiyo bado inatambulika na kwamba hata kwenye vikao vijavyo itaendelea kuzungumzwa ili utekelezaji wake uweze kuendelea na hatimaye kukamilika.

“Niwatoe hofu  kuwa miradi hiyo bado inatambulika na inao umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya wanachi wetu, hivyo hata  kwenye vikao vijavyo  itaendelea kujadiliwa ili tuweze kuona namna ya umaliziaji wake hata kama kwenye bajeti mpya miradi hiyo haipo,” alisema Mgoyi.

Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Halmashauri hiyo Aswege Kaminyoge, alisema kuwa miradi mingi inaonekana kuwa bado haijatekelezwa  kutokana  na  serikali  kutopeleka fedha kwa halmashauri kwa muda muafaka hivyo kupelekea ucheleweshwaji wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Kaminyoge aliongeza kuwa iwapo fedha hizo zitapatikana hakuna mradi ambao ulipitishwa utakaoshindwa kuutekelezwa kwa kuwa ni utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya maendeleo katika halmashauri hiyo.