SIMANZI na majonzi makubwa
yamemkumba Askofu Evarist Chengula(IMC) wa kanisa katoliki la
Mbeya,mapadre,watawa wa kike na kiume pamoja na waumini wote baada ya kumpoteza
aliyekuwa Katibu wa Askofu na mshauri wa Jimbo aliyefariki Okt,4,2012
majira ya saa saba kasorobo nyumbani kwake uaskofuni.
Wingu la vilio na simanzi
limetanda wakati mwili wa Paroko wa kanisa la roho
mtakatifu,Parokia ya Ruanda,Padre Theodorus Johannes Slaats kupokelewa jana
na mapadre,watawa na waumini wa Jimbo la Mbeya waliokuwepo kanisa la Ruanda
kuupokea mwili wake kutoka katika chumba cha kuhifadhia miili ya marehemu
katika Hospitali ya Meta Rufaa, Mbeya majira ya saa 9.00 mchana kwa ajili ya
misa na mkesha hadi leo anapokwenda kuhifadhiwa katika nyumba yake ya milele.
Akizungumzia wasifu wake,Paroko
msaidizi wa Parokia ya roho mtakatifu,Padre Deus Tarimo amesema marehemu padre
Slaats aliyefariki akiwa na umri wa miaka 82 alizaliwa huko
Eindhoven,Uholanzi Novemba,3 mwaka 1930 akiwa ni mtoto wa saba katika familia ya
watoto 12 na kubatizwa siku hiyo hiyo katika kanisa la Mt.Theresia Trudo
huko Uholanzi.
Padre Tarimo amesema marehemu amepata
sakramenti ya kipaimara mei,17,1939,elimu ya msingi katika shule ya
Msingi ya Mt.Theresia mwaka 1937 hadi 1940 na baadaye alihamia katika
shule ya msingi Jan Smitslaan mwaka 1940 hadi mwaka 1943 huko Eindhoven
na baadaye kujiunga na seminari ndogo ya shirika la Roho Mtakatifu,Weert mwaka
1943 hadi 1950.
Alisema baadaye aliendelea na
malezi ya Novisiati katika Shirika hilo huko Gennep Uholanzi mwaka 1950 na
kuweka nadhiri zake za kwanza sept,7,1951 hadi mwaka 1952 alifanya masomo
ya falsafa katika seminari kuu ya Shirika hilo huko Gemert,Uholanzi,masomo ya
Teolojia katika chuo kikuu cha Gregoriana,Roma,Italia (1953-1957),nadhiri
za daima(1954)huko Gemert,Uholanzi,daraja takatifu la ushemasi katika kanisa la
Mt.Marcelli,Roma,Italia(1956).
Padre Tarimo alisema padre Slaats
alipata daraja takatifu la upadre mwaka 1956 ambapo mwaka 1957 alitumwa
kufanyakazi za umisionari nchini Tanzania na utume wake ulianzia Parokia ya
Kisanga,jimbo Katoliki la Morogoro,mwaka 1958 alihudumu Parokia ya Matombo
Morogoro na mwaka 1962 hadi 1964 alikuwa mtratibu Taaluma na mwalimu
katika seminari kuu ya Mt.Thomas,Morogoro huku akifundisha dini katika
chuo cha ualimu kigurunyembe,Sekondari ya Mzumbe na chuo cha Marian kwa
sasa ni Sekondari ya Kilakala.
Alisema marehemu padre Slaats
alihudumu kama Mkurugenzi wa Idara ya Katekesi na afya Jimbo
Katoliki la Morogoro,mwaka 1971 aliombwa na Mhashamu Askofu james Sangu wa
jimbo Katoliki la Mbeya kufanyakazi ya Ukatibu na paroko wa Parokia ya
Mwanjelwa hadi mwaka 1983.
Enzi za uhai wake Padre Slaats
amewahi kuwa Mkuu wa chuo cha ufundi cha Ruanda(1985-1996),mwaka 1997 baada ya
kusimikwa Askofu mpya wa jimbo Katoliki la Mbeya,Askofu Evarist Chengula,
aliteuliwa kuendelea na kazi ya Ukatibu na chansela wa jimbo na
baadaye aliomba kuanzisha Parokia mpya ya Ruanda ambapo Askofu Chengula
alimsimika kuwa paroko mwaka 2003.
Alisema Padre Slaats aligundulika
kuwa na ugonjwa wa kansa mwaka 2004 na kwa nyakati tofauti alikuwa akipata
matibabu katika Hospitali mbalimbali ndani na nje ya Nchi na lakini
aliendelea kujitoa na kuchapa kazi katika nafasi zote hadi alipokwenda
nchini Uholanzi kwa matibabu mwezi januari,mwaka huu na kurudi mwezi juni
na afya yake iliendelea kudhoofika huku akihudumiwa katika Hospitali ya rufaa
Mbeya.
Padre Tarimo alisema
septemba,24,2012 akiwa amedhoofika sana alilazwa katika Hospitali ya Rufaa
Mbeya na kuruhusiwa kurudi nyumbani Oktoba,3,2012 na oktoba,4 aliposhindwa
kuongea na mauti kumfika majira ya saa saba kasorobo mchana katika chumba
chake Uaskofuni,na anatarajiwa kuzikwa kesho katika Parokia ya Ruanda ambako
aliomba ahifadhiwe,Mungu ailaze roho ya marehemu. mahali pema peponi amina.
Habari na Tomson Mpanji Mbeya
