LICHA ya aliyekuwa mwenyekiti wa UWT
wilaya ya Kinondoni, Agnes Luvanda (Mama Makete), kujisalimisha Jeshi la Polisi
Mkoa wa Kinondoni jana, hakuweza kuhojiwa kutokana na kupoteza fahamu ghafla
mara baada ya kuelezwa sababu za kutafutwa kwake.
Habari kutoka chanzo cha ndani ya jeshi hilo,
zimeeleza kuwa baada ya Mama Makete kufika katika kituo cha polisi, Osterbay,
alikutana na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Charles Kenyela, na kuelezwa sababu
za kutafutwa kwake.
Taarifa zinaeleza kuwa baada ya
kufahamishwa madhumuni ya kutafutwa, mama huyo amesema kuwa hawezi kuongea
akiwa peke yake mpaka atakapokuwa na wakili wake hali iliyomfanya Kamanda
Kenyela kumpa fursa ya kumsubiri wakili wake.
Hata hivyo chanzo chetu kilieleza
kuwa akiwa katika chumba cha kusubiria, hali yake ilianza kubadilika ghafla na
kisha kupoteza fahamu jambo lililowafanya askari pamoja na ndugu zake wa karibu
kumuwahisha katika Hospitali ya Masama iliyoko Mbezi Beach kwa matibabu.
