WANAHABARI KUANDANAMA KESHO KULAANI MAUAJI

WAANDISHI wa habari mkoani mbeya  wanatarajia kuungana na waandishi wa habari kote nchini  katika  maandamano  makubwa  ya amani kupinga mauaji  ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Iringa na Mwandishi wa habari wa kituo cha Channel 10, Daud Mwangosi  mnamo Sept,2 mwaka huu yaliyotokea katika Kijiji cha Nyololo mkoani humo.

Maandamano   hayo yatakayowahusisha wanahabari wote mkoani Mbeya yanatarajiwa kuanzia eneo la Mafiat na kumalizikia katika kituo cha mafuta cha zamani cha Bp karibu na Ofisi za Shirika la Nyumba la Taifa(NHC),uhindini, jijini hapa.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari katika ofisi za klabu ya waandishi wa habari (MBPC),mkoani Mbeya maeneo ya uhindini jijini hapa,Katibu wa klabu hiyo, Keneth Mwazembe alisema kuwa  maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika  septemba,11,2012  kuanzia majira ya saa 3.00 asubuhi.

Amesema utaratibu wa kupata kibali kutoka jeshi la polisi unaendelea  baada ya kupeleka maombi   kwa maandishi na kuambiwa warejee saa 8 mchana kupata majibu  kutokana na Mkuu wa polisi wa Wilaya  kudaiwa kuwepo katika kikao.

Hata hivyo Mwazembe amesema kuwa wakati wa maamndamano hayo wanahabari wote watavaa nguo nyeusi ama kufunga kitambaa cheusi mkononi ikiwa ni ishara ya kuomboleza kifo cha mwanahabari mwenzao,wakitembea kimya  bila kelele ikiwa ni njia mojawapo ya kufikisha ujumbe kwa serikali na umma kwa ujumla.