ARUSHA: UVCCM WAKANUSHA MADAI YA KATIBU WA CCM MKOANI HUMO





UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilayani Monduli umekanusha madai ya Katibu wa CCM mkoani hapa, Mary Chatanda kuwa uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali uliegemea misingi ya kundi na kusema walipitisha majina yote kugombea.

Aidha wameeleza mpaka sasa hawajapewa taarifa rasmi juu ya suala hilo pamoja na maelekezo yanayodaiwa kutolewa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho mkoa kilichokaa mwishoni mwa mwezi uliopita zaidi ya kuzisoma kwenye vyombo vya habari.

Mwenyekiti wa UVCCM wilayani Monduli, Julius Kalanga, amesema hayo wakati akieleza mpaka sasa utekelezaji wa maagizo hayo umefikia wapi na kueleza kushangazwa na habari hizo alizozisoma gazetini.

Amesema taarifa hizo hazina ukweli, kwani hakukuwa na kitu kama hicho wao walipitisha majina yote ya wale waliojitokeza kugombea nafasi ya uenyekiti wa UVCCM wilaya.