VIKWAZO VYAZIDI KUONGEZWA SYRIA

Viongozi mbalimbali duniani wameutaka Umoja wa Mataifa kuongeza shinikizo kwa Rais Bashar al- Assad wa Syria ili aachie madaraka. 

 Mataifa 100 na taasisi mbalimbali ambazo zimekutana mjini Paris kwa mazungumzo, zimelitaka Baraza la Usalama la Umoja huo kulifanyia kazi suala la kuundwa kwa serikali ya mpito nchini humo na kupendekeza kuwekwa vikwazo kama Assad atakaa mpango huo. 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Hillary Clinton ametoa wito kwa nchi mbalimbali kuendelea kushinikiza mabadiliko ya utawala yafanyike Syria ili kumaliza mzozo uliodumu kwa miezi 16.

Ameikosoa Urusi na China kwa kuzorotesha mpango huo. Mkutano huo wa Paris umeingiliana na taarifa  kuwa jenerali mmoja mwandamizi  amekimbia  jeshi la Assad jambo ambalo ni pigo kubwa kwa utawala huo.