ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Hawa Ng’umbi, amewasilisha hati ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa nchini, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambayo ilitupilia mbali kesi yake ya uchaguzi ambayo ilikuwa ikipinga ubunge wa John Mnyika (CHADEMA).
Nia hiyo imewasilishwa Mahakama ya Rufaa na wakili wake, Issa Maige, kwa njia ya maandishi ikiwa ni siku chache baada ya Jaji wa Mahakama Kuu, Upendo Msuya kutupilia mbali kesi ya uchaguzi Na. 107 ya mwaka 2010.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi, Ng’umbi amethibitisha kuwasilisha kusudio hilo la kukata rufaa na kwamba tayari nakala ya kusudio hilo amekwisha kupelekewa Mnyika.
