WAHUDUMU MATATANI BAADA YA N/WAZIRI KUFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA

Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mh. Dk.Hamisi Kigwangalla ameendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua huduma za Afya ‘Imarisha Afya’ katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali mbalimbali kwenye Mikoa ya Rukwa, Katavi pamoja na Tabora.
Akiwa katika mkoa wa Rukwa, Dk. Kigwangalla aliweza kutembelea Hospitali ya Sumbawanga ambayo ni ya Mkoa wa Rukwa na kujionea mambo mbalimbali huku akiwapongeza kwa namna walivyoboresha huduma zao ikiwemo ile ya Maabara, Chumba cha upasuaji na huduma zingine ambapo aliwaagiza kuhakikisha wanakuwa na hakiba ya kutosha ya damu salama kwa ajili ya dharura kwa wagonjwa wa ukanda huo.
Mbali na Hospitali ya Mkoa wa Rukwa, pia aliweza kutembelea kituo ca Laela ambapo pia mbali ya kujionea utendaji kazi wa kituo hicho alipongeza juhudi za Mbunge wa jimbo la Kwera, Mh. Ignas Alloyce Malocha kwa kushirikiana na wananchi wake katika masuala ya huduma za Afya.
Ziara hiyo katika mkoa wa Rukwa, aliweza kumalizia katika Kituo cha Afya Wampembe kilichopo Wilayani Nkasi ambapo alijionea shughuli mbalimbali ikiwemo huduma za Upasuaji hata hivyo aliutaka uongozi wa kituo hicho ambacho kipo mwambao wa Ziwa Tanganyika kuhakikisha wanakamilisha mifum ya maji safi na salama ndani ya kituo pamoja na kuboresha huduma za Maabara na usafi kwa ajumla.
Akiwa katika Mkoa wa Katavi, Dk. Kigwangalla aliweza kufanya ziara ya kushtukiza kituo cha Afya Inyonga,kilichopo Mlele majira ya Saa Sita mchana na kuweza kukagua maeneo mbalimbali ikiwemo Chumba cha Maabara, Chumba cha Upasuaji na wodi ya akina mama wanaosubiria kujifungua.
Hata hivyo, Dk. Kigwangalla amemtaka Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo hicho kumuandikia maelezo juu ya kutokuwepo kwa watoa huduma kwenye jengo la chumba cha upasuaji na eneo la wodi ya akina mama wanaosubiria kujifungua kwani licha ya kufika hapo hakukuta mtoa huduma hata mmoja kwa wakati huo hali ambayo inaweza kuleta hatari.
“Nataka kupata maelezo kwa maandishi. Kwa nini hakukua na watoa huduma ndani ya Chumba cha upasuaji na kule kwa wodi ya wamama wajawazito. Nilifika kuwakagua kwa upande wa Maabara nimekuta safi mumeweza kuboresha huduma na mumezingatia maelezo yangu niliyoyatoa kipindi nilichofika kukagua mwaka jana. Lakini pia hali niliyoikuta katika maeneo hayo niliyotembelea bila kuwakuta wahusika hii ni hatari nitahitaji maelezo ya kimaandishi” alieleza Dk. Kigwangalla wakati akitoa maagizo kwa Kaimu Mganga Mkuu wa kituo hicho.
Aidha, akiwa katika mkoa wa Tabora, aliweza kutembelea eneo la jengo linalojengwa Hospitali ya Wilaya ya Uyui na baadae aliweza kumalizia ziara yake katika Zahanati ya Isikizya ambapo aliagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Uyui kuhakikisha wanatenga bajeti pamoja na kushirikiana na nguvu za wananchi na mbunge wa jimbo hilo wanajenga majengo ya kulazwa wagonjwa, chumba cha upasuaji, maabara na miundombinu mingine ili Zahanati hiyo ije kupanda na kuwa Kituo cha Afya kwani kinahudumia eneo kubwa katika mji huo wa Isikizya ambayo hipo ndani ya Makaomakuu ya Wilya hiyo.
Mwisho.

from Blogger http://ift.tt/2eDoFeF
via IFTTT