SERIKALI YAWAKANYA MAAFISA ARDHI NA MAAFISA MIPANGO MIJI

Na Hassan Mabuye Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ardhi
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amewaonya maafisa ardhi na maafisa mipango miji wasio waadilifu na kusababisha kero za migogoro ya ardhi nchini.
Waziri Lukuvi aliyasema hayo leo katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Lugalo mjini Iringa wakati wa Uzinduzi wa Master Plan ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Amesema mchezo huo wa ufisadi ambao umekuwa ukitumiwa miaka yote na maofisa ardhi nchini ameubaini na kuwataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kutokubaliana na ramani za maeneo mapya zinazoletwa na wataalam hao bila ya wao kufika maeneo husika na kuoneshwa maeneo hayo ili kujiridhisha.
Waziri Lukuvi amefichua kuwa ufisadi unaofanywa na maafisa ardhi nchini kwa kupima viwanja hewa kwa ajili ya maslahi yao na kusema kuwa mbinu ambayo wamekuwa wakiitumia kuiibia serikali amekwisha ibaini na hata kubali kuona mbinu hiyo inapewa nafasi katika serikali hii ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli .
Maafisa ardhi wakishirikiana na maafisa mipango miji pamoja na wapima wamekuwa wakitajirika sana kwenye idara zao na wanatakata kwa ujanjaujanja na ufisadi wanaoufanya kwa kutengeneza ramani zinazoonesha maeneo mazuri na muhimu katika miji kwamba hayafai kutumika, kumbe wameyauza maeneo hayo kwa mlango wa nyuma na kwa bei za juu.
Unakuta kwenye ramani inayonyesha kuna bonde kubwa lisilofaa kujengwa kumbe ukifuatilia eneo hilo ni zuri kuliko yote na hapo wametenga viwanja vya kuuza. Unakuta ukipima kuna viwanja vingi na vizuri ambavyo ni vyao wao wanachofanya baada ya kuuza viwanja halali za Halmashauri hurudi kupima maeneo hayo walioonyesha ni mabonde na kugawana wao kwa ajili ya kuuza kwa faida yao.
Lukuvi amesema kuwa wathamini nao pi wamekuwa wakiwapunja wananchi wasio elewa kwa kuwafanyia tathimini kubwa zaidi ya uhalisia wake na pindi pesa inapotoka utakuta nyumba inathamani ya milioni 7 wakati wao wanasema inathamani ya milioni 20 ili cha juu wapate wao.
“Wakati nilipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam niliweza kubaini ujanja wa wathamini baada ya eneo ambalo nyumba zake zina thamani kati ya milioni 20 hadi 50 kwa maana nyumba hizo ni za udongo ila maofisa hao walimtafuta mtu na kutafuta nyumba nzuri zaidi na kumshikisha kibao kisha kumpiga picha na kuandika kuwa nyumba hiyo inathamani ya zaidi ya milioni 200.”
Niliamua kufanya uchunguzi wangu na kumtafuta mtu aliyekwenye picha na kumbana ndipo aliniambia ukweli kuwa mthamini huyo ni ndugu yake hivyo walikubaliana pesa ikitoka atalipwa milioni 70 na milioni 130 ni za afisa huyo”
Hata hivyo alisema kuwa ujenzi holela katika miji na halmashauri imesababishwa na ukilitimba wa utoaji wa vibali kwa wakati na ndio sababu ya wananchi kuvamia maeneo yasiyo pimwa japo kuanzia sasa wote waliopo katika maeneo yasiyo pimwa watapewa leseni ya makazi ya miaka mitano na watalipa kodi ya ardhi na baada ya miaka mitano wahakikishe wamepimiwa ili kupewa hati.
Hivyo Lukuvi aliwataka maafisa ardhi na wathamini wa ardhi manispaa ya Iringa kutofanya kama maeneo mengine kwa kufuata mpango maeneo yote ambayo yameelekezwa kwenye Masta Plan hiyo na kwenda kutenda haki.
Katika hatua nyingine waziri Lukuvi alitoa agizo kwa wale wote waliopewa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa hoteli na viwanda na wale waliouziwa viwanda vya serikali, hotel na mashamba ya serikali kuviendeleza haraka kabla ya ardhi hiyo haijapokonywa .
Nae Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bibi Amina Masenza akimkaribisha waziri Lukuvi amesema kuwa mkoa wa Iringa umeendelea kuhamasisha wananchi kuzingatia sheria na taratibu za ujenzi na kuachana na ujenzi holela na ndio sababu ya kuja na Masta Plan hiyo ambayo imeanzishwa na aliyekuwa mstahiki meya wa halmashauri hiyo Amani Mwamwindi.
Akitoa taarifa ya uandaaji wa Masta Plan hiyo kwa ajili ya mwaka 2015-2035 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Dkt William Mafwere, alisema kuwa dhumuni la mpango huo ni kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili Manispaa na kuwa dhana kuu ya mpango huo ni dhana unganishi ikijumuisha dhana nyingine.
Alisema jumla ya miradi 31 itatekelezwa katika awamu ya kwanza 2015-2020 kuwa baadhi ya miradi hiyo ni kituo cha mabasi Igumbilo, kituo hicho kimeanza ujenzi na hatua ya utekelezaji imefikia asilimia 30.
Nae Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa alisema kuwa kazi inayofanywa na Waziri Lukuvi ni tofauti na mawaziri wengine kwani amekuwa ni waziri wa mfano katika kuchapa kazi.
“Kwa mnaonifahamu vizuri mimi sio mbunge wa kusifia sifia ni mbunge mwenye msimamo ila nampongeza sana Waziri Lukuvi ni waziri mchapakazi na kazi zake zinaonekana na ndio maana hata bungeni ni waziri pekee ambaye bajeti yake ilipitishwa kwa kishindo hata na sisi wabunge wa kambi ya upinzani.”
Mpango Kabambe ni chombo cha kuchochea utumiaji wa fursa zilizopo katika mji, kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kupunguza na kumaliza migogoro ya ardhi. kudhibiti ujenzi holela mijini na hutumika pia kuongoza, kusimamia na kudhibiti ukuaji na uendelezaji wa mji na kutoa uhakika kwa wawekezaji katika Halmashauri za Manispaa ya husika.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwaonya maafisa ardhi na maafisa mipango miji wasio waadilifu na kusababisha kero za migogoro ya ardhi nchini wakati wa uzinduzi Master Plan ya mji wa Iringa.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimkabidhi kitabu cha Master Plan ya mji wa Iringa Meya wa Halmashauri ya Iringa Alex Kimbe.


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiteta jambo na Meya wa Halmashauri ya Iringa Alex Kimbe na Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akipongezwa na Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa mara baada ya Uzinduzi wa Master Plan ya mji wa Iringa.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Iringa waliofika kushuhudia Uzinduzi huo.

from Blogger http://ift.tt/2tytLPX
via IFTTT